Upepo waezua mapaa ya madarasa, wanafunzi wakatisha masomo

Musoma. Wanafunzi 201 wa Shule ya Msingi Mkiringo iliyopo Wilaya ya Butiama mkoani Mara, wamebaki bila pa kusomea baada ya upepo mkali kuezua mapaa ya madarasa.

Tukio hilo lilitokea jana Agosti 28, 2024 saa 1:00 usiku, upepo huo ukiambatana na mvua kubwa. Mwenyekiti wa Kamati ya Shule, Chacha Warioba amesema jumla ya madarasa matatu yameezuliwa na hayataweza kutumika kwa sasa.

“Haya madarasa yalikuwa yakitumiwa na wanafunzi wa darasa la tatu na la nne, lakini kutokana na hali ilivyo, leo wanafunzi hawajaweza kuingia darasani, hivyo vipindi vya leo vimepotea na watoto wanacheza tu nje,” amesema.

Amefafanua kuwa upepo mkali pamoja na mvua iliyonyesha kwa takriban dakika 30 haukusababisha madhara kwa binadamu kwa sababu tukio hilo lilitokea wakati wanafunzi na walimu hawakuwepo shuleni.

Uongozi wa serikali ya kijiji na kamati ya shule unatarajiwa kukutana baadaye leo ili kujadili hatua za dharura zinazohitajika kurejesha hali ya kawaida shuleni hapo.

Diwani wa Nyankanga, Jacob Shangire, akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti 29, 2024, amesema kabla ya tukio hilo, shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 800 ilikuwa tayari na upungufu wa madarasa manane, hivyo tukio hilo limeongeza changamoto ya ukosefu wa madarasa.

“Kama unavyojua, tuko kwenye mitihani na kutokana na tukio hili, leo wanafunzi wameshindwa kufanya mitihani kwa kuwa hakuna madarasa hata ya dharura, ukizingatia tulikuwa na upungufu wa madarasa, ndio maana wanafunzi 200 walikuwa wanatumia madarasa mawili tu,” amesema Shangire.

Ameongeza kuwa hii ni mara ya tatu madarasa ya shule hiyo yanaezuliwa mapaa, Desemba mwaka jana, madarasa matatu yaliyokumbwa na tukio kama hilo, yalikarabatiwa na kuanza kutumika tena.

Mwaka juzi pia madarasa mengine yaliezuliwa. Ameeleza kuwa chanzo cha matukio haya ni uchakavu wa majengo ya shule hiyo.

“Hapa panahitajika ukarabati mkubwa kwa sababu haya madarasa ni ya muda mrefu, ndio maana kila mara yamekuwa yakiezuliwa. Bahati nzuri matukio yote yametokea wakati walimu na wanafunzi hawapo shuleni, la sivyo, madhara yangekuwa makubwa zaidi,” amesema.

Ameiomba Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kutoa fedha za dharura ili kurejesha miundombinu ya madarasa hayo kusudi wanafunzi waendelea na mitihani, huku ikifanyika mipango ya ukarabati mkubwa.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mkiringo wamesema tatizo hilo linapaswa kushughulikiwa haraka ili wanafunzi wapate nafasi ya kufanya mitihani yao.

“Tunaelekea kipindi cha mvua, hivyo wananchi na serikali tunapaswa kushirikiana kufanya ukarabati utakaoyafanya majengo haya ya madarasa kuwa imara na kuhimili msimu wa mvua na kuepuka madhara yanayoweza kutokea kutokana na uchakavu uliopo sasa,” amesema Gerald Magibo anayeishi jirani na shuke hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele ameliambia Mwananchi kuwa ametoa wiki mbili kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama kufanya ukarabati wa madarasa hayo yaliyoezuliwa.

Ameongeza kuwa shule hiyo tayari iko kwenye mpango wa maboresho makubwa ambayo yanatarajiwa kuanza hivi karibuni, ingawa hakuweza kutaja ni lini.

“Nimefika shuleni na kubaini upungufu mwingi. Pamoja na mpango wa muda mfupi, shule hii ni miongoni mwa shule zinazotarajiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa na kubadilishwa kuwa mpya kabisa,” amesema Kaegele.

Related Posts