Shinyanga. Viungo vinavyodhaniwa kuwa vya mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Tinde B mkoani Shinyanga, Junior Maganga (7) vimeonekana wilayani humo, baada mtoto huyo kupotea tangu Agosti 22, 2024.
Akithibitisha tukio hilo leo Alhamisi Agosti 29, 2024 Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi amesema tukio hilo limetokea Agosti 27, mwaka huu katika Kijiji cha Jomu Kata ya Tinde.
Hata hivyo taarifa zaidi zitatolewa na makao makuu ya jeshi hilo baada ya uchunguzi kufanyika.
Diwani wa kata ya Tinde, Jafari Kanoro amesema mtoto huyo alipotea Alhamisi, Agosti 22, 2024 na ilipofika Jumatatu ya Agosti 26, 2024 waliona mguu mmoja kwenye Kitongoji cha Chabayanda, huku fuvu la kichwa, koromeo na nguo vimekutwa Kijiji cha Jomu kitongoji cha Malenge Agosti 27.
“Fuvu la kichwa, nguo na yebo vimegunduliwa na mchunga ng’ombe (hakumtaja) alitoa taarifa kwenye uongozi wa Kitongoji cha Malenge na tayari Jeshi la Polisi limepewa taarifa na kuja kuchukua viungo hivyo Pamoja na nguo kuondoka navyo,” amesema Kanoro.
Mtendaji wa Kijiji cha Jomu, Cheyo Maganga amesema kwa mujibu wa taarifa za mzazi mwa mtoto huyo, usiku wa siku aliyopotea alimtuma maji ndani ya nyumba nyingine lakini hakurudi hadi walipoona viongo vyake.
“Lakini baada ya kuripoti tukaanza zoezi la kumtafuta ndipo hiyo siku tukaona fuvu la kichwa, nguo na yebo na akamwita mzazi wa mtoto huyo na akabaini vitu hivyo ni vya mwanaye,”amesema Maganga.
Amesema pamoja na mzazi kukubali kuwa nguo hizo ni za mtoto wake, alivitambua pia vidole ambavyo vilikuwa havina michubuko kuwa ni vya mtoto wake.