Wandewa wanaingia, Yanga | Mwanaspoti

“EEEH! Wandewa wanaingia … Ooh wenye mji wamevamia.” Hiyo ni mistari iliyopo katika ngoma moja matata ya Achii aliyoimba Diamond Platinumz akimshirikisha Koffi Olomide.

Baada ya kushuhudiwa mechi 10 za Ligi Kuu Bara, leo zinapigwa mechi mbili ikiwamo ile itakayokutanisha watetezi, Yanga dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba ma mapema KMC itakuwa wenyeji wa Coastal Union.

Timu hizo zitakutana, huku rekodi zikiwabeba Yanga mbele ya wageni wao, kitu kinachofanya mashabiki kutaka kujua watetezi hao wataanza na gia gani baada ya msimu uliopita kutetea ubingwa kwa msimu wa tatu mfululizo ambapo Kocha Miguel Gamondi kuna kitu anajivunia nacho.

Yanga itavaana na Kagera iliyotoka kupoteza mechi ya kwanza dhidi ya S8ingida Black Stars kwa bao 1-0 wikiendi iliyopita, huku Gamondi akijiamini zaidi baada ya kuuanza msimu akibeba Ngao ya Jamii mbele ya Simba na Azam alizozifunga, kisha akatinga raundi ya  pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiichapa Vital’O ya Burundi jumla ya mabao 10-0.

Akilini mwa Gamondi ambaye moto wa Ligi Kuu anaanza kuuwashia ugenini, anafahamu kwamba malengo ya klabu ni yaleyale kubeba ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo.

Msimu uliopita Gamondi ikiwa ni mara ya kwanza kufundisha Yanga alienda Kaitaba kucheza na Kagera  mjini Bukoba na kutoka suluhu, lakini mechi ya marudiano Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam, alishinda 1-0 dakika za jioni kupitia Mudathir Yahya.

“Tunahitaji kufikiria kuhusu sasa. Nasema kila mchezo ni tofauti. Msimu uliopita ilibaki kidogo tupoteze pale (Kaitaba). Nakumbuka vizuri mchezo huo. Lakini sasa hali ni tofauti,” alisema Gamondi.

Kocha huyo raia wa Argentina, amebainisha kwamba msimu uliopita alipokwenda kucheza dhidi ya Kagera Sugar, alikuwa hawafahamu vizuri wapinzani wake, lakini sasa ana mafaili yao yote na anajua namna ya kudili nao.

“Sasa tuna taarifa kuhusu Kagera, tunajua hali yetu na tutakwenda kwa ushindi. Sifikirii kuhusu kilichotokea hapo awali. Nafikiri tuko tayari kwa vita ingawa itakuwa ngumu kwa sababu uwanja ni mgumu,” alisema Gamondi na kuongeza.

“Kwa hakika Kagera na timu zote zinazocheza dhidi ya Yanga zinajitoa kwa zaidi ya asilimia 200. Lakini tuna imani sisi wenyewe. Tusiwaze kuhusu kilichotokea hapo awali. Tusiwaze kuhusu sisi kuwa mabingwa. Tuangalie hapa tulipo. Tunajua sisi ni timu nzuri sana, lakini tunahitaji kuthibitisha hilo kila siku. Nina imani tutakwenda kupata pointi tatu.”

Kocha Paul Nkata anayeinoa Kagera ikiwa ni msimu wa kwanza, baada ya kupoteza mchezo wa kwanza anaamini leo itakuwa ni sehemu ya kurekebisha makosa yao, huku akiwategemea nyota kadhaa wazoefu wa ligi hiyo kama Obrey Chirwa, Nassor Kapama, Cleophas Mkandala, Deo Mafie, David Luhende, Samuel Onditi na Joseph Mahundi kuibana Yanga itakayomkosa beki wa kulia Yao Kouassi aliye majeruhi.

REKODI ZINASEMAJE?
Rekodi zinaonesha, Yanga mara ya mwisho kucheza Kaitaba katika mechi ya Ligi Kuu matokeo yalikuwa 0-0, ilikuwa Februari 2, 2024. Kumbukumbu nzuri iliyopo kwa Yanga ndani ya Kaitaba ni ushindi mnono wa mabao 6-2 ilioupata Oktoba 22, 2016.

Ukiangalia rekodi za jumla kwa misimu kumi iliyopita, Yanga ikiwa ugenini dhidi ya Kagera imecheza mechi kumi na kushinda nane, sare moja sawa na ilivyopoteza.

Katika mechi hizo kumi za ugenini dhidi ya Kagera, Yanga imefunga mabao 16 na kuruhusu nyavu kuguswa mara nne, huku ikiambulia clean sheet saba.

Kwa ujumla, Kagera na Yanga katika misimu kumi iliyopita ndani ya Ligi Kuu pekee, zimekutana mara 20, Kagera imeshinda mbili sawa na sare zilizopatikana, huku Yanga ikishinda 16. Yanga inaongoza kwa kufunga mabao mengi dhidi ya Kagera katika kipindi hicho ikiwa nayo 41 wapinzani wao wakifunga 16.

KMC VS COASTAL
Ni mchezo mwingine utakaochezwa leo saa 10 jioni kwenye Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam wenyeji KMC watawakaribisha Coastal Union, huku rekodi zikionyesha zinapokutana kumekuwa na matokeo mengi ya sare. Mara ya mwisho kukutana msimu uliopita ambapo nyumbani na ugenini timu hizo zilishindwa kufunga na leo zitafungua msimu kila mojka ikicheza mechi ya kwanza, Waghosi wakitoka kutolewa Kombe la Shirikisho Afrika na AS Bravos ya Angola kwa mabao 3-0.

Tangu msimu wa 2018/19 ambapo KMC ilianza kushiriki Ligi Kuu Bara, imekutana na Coastal mara 12, huku matokeo ya sare yakiwa saba, ushindi kwa Coastal ni tatu na KMC ikishinda mbili ikiwemo ushindi mnono wa mabao 5-2 ilioupata msimu wake wa kwanza.

Kocha wa KMC, Abdi Hamid Moallin, alisema: “Ni mchezo wetu wa kwanza wa ligi, naamini utakuwa mgumu lakini wachezaji wapo tayari tukifahamu kwamba ligi ni ngumu, tutatumia faida ya uwanja wetu wa nyumbani kusaka matokeo mazuri.”

Ngawina Ngawina anayeinoa Coastal Union alisema wapinzani wao katika msimu uliopita walikuwa moto katika mashindano hayo na kwamba, wamejipanga kupambana nao ipasavyo.

 “Msimu uliopita KMC walimaliza ligi nyuma yetu kwa nafasi moja, tunawaheshimu wana mwalimu mzuri na kikosi kizuri, tumejipanga kukabiliana nao kwani tunawafahamu vizuri,” alisema.

Related Posts