Dodoma. Madeni ya jumla ya Sh21.7 bilioni ya wazabuni wa vyakula katika shule za msingi na sekondari kwa mwaka 2023/24 yamewasilishwa hazina kwa ajili kuhakikiwa na kulipwa.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Agosti 29, 2024 na Naibu Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Bernadeta Mushashu.
Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali italipa madeni ya wazabuni wanaotoa huduma za vyakula kwenye shule mbalimbali tangu mwaka 2023 hadi 2024.
Akijibu swali hilo, Katimba amesema Serikali imekuwa ikipokea madeni mbalimbali ya wazabuni wa chakula kwa shule za msingi na sekondari za Serikali kutoka katika halmashauri zote.
“Madeni hayo yamekuwa yakilipwa baada ya uhakiki na kadiri ya upatikanaji wa fedha. Mwaka 2020/21 – 2022/23 Serikali imelipa wazabuni wa chakula shuleni kiasi cha Sh26.3 bilioni,” amesema.
Amesema mwaka 2023/24 Ofisi ya Rais –Tamisemi imekusanya madeni ya wazabuni wa chakula katika shule za msingi na sekondari yenye jumla ya Sh21.7 bilioni (shule za msingi Sh761.8 milioni na Sekondari Sh20.9 bilioni).
Katimba amesema madeni hayo yamewasilishwa hazina kwa ajili ya taratibu za uhakiki na malipo.
Katika swali la nyongeza, Bernadeta amesema fedha zinazotengwa kumlisha mwanafunzi kwa siku ambazo ni Sh1,500 hazitoshi kumpa mlo kamili kwa maana mlo wenye virutubisho kamili.
“Je Serikali ina mpango gani wa kuongeza kiasi kusudi kiweze kulingana na hali halisi ya maisha,” amehoji mbunge huyo.
Pia amesema madeni ya wazabuni shuleni bado ni makubwa na mengine yako katika halmashauri hayajafika hata wizarani.
“Serikali mnampango gani wa kuhakikisha sasa wakuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha madeni hayo yanalipwa kila mwezi yasiendelee kurundikana kule,” amehoji.
Akijibu swali hilo, Katimba amesema kiwango cha chakula kwa mwanafunzi mmoja kila siku kimeboreshwa kutoka Sh1,500 hadi Sh2,000.
Amesema Serikali itakuwa inahakikisha kwa kadri muda unavyokwenda na bajeti inavyoruhusu inafanya mapitio ya gharama hiyo ili kuiboresha zaidi.
“Tamisemi itaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha kuhakikisha fedha zote zitakazokuwa zimetengwa zinatolewa zote kulingana na idadi ya wanafunzi wa bweni walioko katika shule hizo,” amesema.
Ametoa maagizo kwa mamlaka za Serikali za mitaa nchini ambazo zina shule za bweni kufanya uhakiki wa madeni yote ya wazabuni wa chakula na kuwasilisha Tamisemi na wao wawahishe Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo.