Aenda jela miaka 30 kwa kumbaka mtoto wa miaka 13

Mufindi. Frank Kahise, mkazi wa Mtaa wa Mkombwe amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Mufindi, Iringa, kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka 13.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mfawidhi Benedict Nkomola Agosti 21, 2024, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuwa alitenda kosa hilo Juni 6, 2024, katika nyumba ya kulala wageni huko Mtaa wa Mkombwe, kata ya Boma, kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(e) na 131(1) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano, akiwemo mwathirika mwenyewe na mshtakiwa alijitetea mwenyewe.

Mahakama ilielezwa kuwa siku ya tukio, mtoto huyo alisafiri na mshtakiwa kutoka Dodoma kwa lengo la kutafutiwa kazi. Walipofika Mafinga, walichukua vyumba viwili katika nyumba ya wageni, lakini usiku mshtakiwa alienda kumgongea mlango binti huyo, akamwingilia kimwili kwa nguvu.

Siku iliyofuata, mshtakiwa alimhamishia binti huyo kwenye nyumba nyingine ya wageni na akaendelea kumbaka kabla ya kuondoka akidai kwenda kumnunulia nguo.

Mhudumu wa nyumba hiyo ya wageni alitoa taarifa kwa uongozi wa mtaa na hatimaye Kahise alikamatwa.

Baada ya kusomewa hati ya mashtaka, Kahise alikana, lakini ushahidi ulithibitisha shtaka hilo na kuishawishi Mahakama.

Kabla ya hukumu kutolewa, Wakili wa Serikali Simon Masinga aliomba adhabu kali itolewe kwa mshtakiwa ili iwe funzo kwa wengine. Mahakama pia iliamuru mtoto huyo awe chini ya usimamizi wa ustawi wa jamii kwa ajili ya msaada zaidi.

Related Posts