WIKI kadhaa zilizopita niliandika hapa kuwa kuna mpango wa Coastal Union kuachana na kocha David Ouma kutoka Kenya kwa kile kilichotajwa kuwa uongozi hauridhishwi na namna anavyolisimamia benchi la ufundi la timu hiyo.
Na katika hilo andiko nilishauri Coastal isifanye hivyo kwa kocha huyo kwa vile ingejiweka katika uwezekano wa kutofanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Labda walikaa wakashauriana na kuamua kubaki naye baada ya msimu uliopita kumalizika lakini inaonekana ndani ya nyoyo zao tayari walikuwa wanasubiria jambo fulani tu litokee ili wamtimue.
Na kweli imetokea baada ya kocha huyo kutimuliwa muda mfupi baada ya Coastal kupoteza kwa mabao 3-0 mbele ya Onze Bravos ya Angola katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Lakini matokeo hayo ni kama sababu tu ya kusimama mbele ya vyombo vya habari ila uhalisia ni kwamba baadhi ya viongozi wa Coastal walikuwa wanamnyooshea kidole Ouma kuwa alishindwa kuwafanya wachezaji wa timu hiyo kuwa fiti.
Inatajwa kwamba hakuwa akipenda wachezaji wa Coastal wafanye mazoezi ya kutosha ambayo yangewafanya wawe fiti na muda mwingi alikuwa anajikita na kuwafanyisha mazoezi ya mbinu tu.
Ingekuwa kama hakuna sababu nyingine nyuma ya pazia, sidhani ingemtimua Ouma mara baada ya kupoteza kwa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Onze Bravos kwa sababu ni matokeo ambayo hayakuwa ya kushangaza kutokana na uhalisia.
Timu ilikuwa imetoka kufanya usajili wa wachezaji kadhaa wapya ambao walihitaji muda wa angalau miezi miwili ili waweze kukaa sawa na kutengeneza muunganiko wa kitimu jambo ambalo halikuwepo kwa Coastal.
Haya yote naamini viongozi wa Coastal wanayafahamu lakini kiuhalisia tayari ilishakuwa na sababu ya muda mrefu ya kuachana na kocha huyo lakini iliamua kutafuta sehemu ya kumbana tu.