Moshi. Askofu Fredrick Shoo wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amekemea vikali vitendo vya kikatili vinavyohusisha mauaji yanayodaiwa kuwa na viashiria vya ushirikina, utekaji na matumizi mabaya ya nguvu na mamlaka, ambavyo vinatishia usalama wa nchi.
Dk Shoo, ambaye pia ni mkuu mstaafu wa KKKT, amezungumzia pia wizi wa kura na rushwa wakati wa uchaguzi, akiwataka Watanzania kuomba Mungu ili kuliepusha Taifa na vitendo hivyo.
Ameyasema hayo leo Ijumaa, Agosti 30, 2024, wakati akifungua mkutano mkuu wa 38 wa Dayosisi ya Kaskazini uliofanyika katika Hoteli ya Uhuru, Mjini Moshi.
Akielezea kwa masikitiko, Askofu Shoo amesema vitendo hivyo vya kikatili, ikiwa ni pamoja na mauaji na utekaji, vinaweza kuhusishwa na masuala ya uchaguzi, jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa nchi.
Ameongeza kuwa, ikiwa mauaji hayo yanahusishwa na uchaguzi kwa lengo la kujipatia nafasi za uongozi, wale wanaohusika wanapaswa kumuomba Mungu, kwani ikitokea kwamba wanapata nafasi hizo, Taifa litaingia kwenye vilio na majonzi.
“Biblia inasema kiongozi mwovu anapotawala, nchi huugua. Hivyo, viongozi wanaotumia njia za ushirikina kujipatia madaraka wamesahau kuwa madaraka na mamlaka vinatoka kwa Mungu. Ikiwa mtu huyu atapata madaraka, nchi italia.
“Tunahitaji kuomba sana na kuwakataa wote wanaotumia njia za kikatili kumwaga damu za watu ili kujipatia madaraka, mali, na vyeo mbalimbali,” amesema.
Aidha, ameendelea kukemea vitendo vya wizi wa kura, rushwa wakati wa uchaguzi, ulevi na ufujaji wa mali za umma, akisema vitendo hivyo vinaweza kuharibu sifa ya Taifa na kuleta laana.
Amesisitiza kuwa ni lazima Watanzania wote wakatae mambo hayo na kuwakataa viongozi wanaohusika ili kuhakikisha wanapatikana viongozi bora na si bora viongozi.
“Tanzania katika karne hii ya 21 kuelekea karne ya 22 bado tunapambana na changamoto kama madawati shuleni, matundu ya vyoo, madarasa na upungufu wa dawa, huku mchwa wakiendelea kutafuna fedha za umma na kuwaacha Watanzania wenzao katika hali mbaya. Ni wakati wa kila mmoja kukataa na kukemea wizi na ubadhirifu wa mali za umma,” amesema.
Dk Shoo pia amewataka wananchi kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura na wale wenye sifa za uongozi kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali.
Amesisitiza umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu 2024, na Uchaguzi Mkuu 2025, ili kuwachagua viongozi bora bila kujali itikadi za kisiasa.
Kwa upande wake, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Msafiri Mbilu amewahimiza viongozi wa Dayosisi ya Kaskazini kufanya kazi kwa bidii, kuwa waaminifu katika kutunza muda na mali za kanisa na kuondokana na umaskini.
“Tuwe waaminifu katika kutunza muda, kutunza mali za kanisa. Tumekabidhiwa mali nyingi, tuwe waaminifu,” amesema Askofu Mbilu.