Moshi. Mkutano Mkuu wa 38 wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) umemrudisha Askofu Fredrick Shoo kuwa mkuu wa dayosisi hiyo kwa kipindi maalumu cha miaka sita.
Askofu Shoo alichaguliwa kuiongoza Dayosisi ya Kaskazini Agosti 2014 na mwaka huu amemaliza vipindi vyake viwili vya uongozi lakini mkutano mkuu kupitia mapendekezo ya halmashauri kuu, ukamuomba kuendelea katika kipindi kingine cha miaka sita kwa sababu maalumu.
Akizunguza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Zebadiah Moshi amesema Halmashauri kuu katika kikao chake cha 249 cha Agosti 30, 2024 kimeridhia na kupendekeza kwa mkutano mkuu wa 38 wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini kumuomba Dk Fredrick Shoo akubali kuendelea kuongoza Dayosisi hiyo kwa kipindi maalumu cha miaka sita
“Kwa mujibu wa katiba, halmashauri kuu imeridhia na kinapendekeza kwa mkutano mkuu wa 38 wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini kumuomba Baba Askofu Fredrick Shoo akubali kuendelea kuongoza Dayosisi kwa kipindi maalumu cha miaka sita”
Amesema Askofu Shoo Mungu amemjalia afya, nguvu na maono ya uongozi ambayo Dayosisi hiyo bado inahitaji.
Amesema “Hatua hiyo pia itasaidia kutimiza ndoto na azma ya dayosisi katika miradi mbalimbali ambayo inaendelea na kuendelea kuimarisha mahusiano yaliyokuwepo na aliyoyaanzisha kati ya Dayosisi na wadau mbalimbali wa maendeleo ndani na nje ya nchi”
Ameongeza kuwa “Pia ataendelea kuwakuza na kuwajengea uwezo viongozi vijana kwa ajili ya kuchukua nafasi za uongozi siku za usoni, pia Askofu anazo nafasi za uongozi alizochaguliwa ikiwemo CCT na fungamano la makanisa ya Kilutheri duniani hivyo hii ni heshima kwetu dayosisi.”
Akizungumza baada kurudishwa kuwa Mkuu wa Dayosisi hiyo, Dk Shoo amesema anaendelea kumshangaa Mungu kwa wema wake na ukuu wake wakati wote na kuwaomba waumini wa Kanisa hilo kuendelea kumuombea.
“Nilisema niite nami nitaitika, nitume nami nitaenda, sijawahi kutafuta kwa njia yoyote ile nafasi katika utumishi huu, kwa hiyo mimi ninaamini na ndicho kiapo changu tu kwamba Mungu amewatumia ninyi kuweka ombi hili kwangu na familia yangu.”
“Nimeshauriana na mpenzi mke wangu na watoto, na mama amenikumbusha hujawahi kutafuta, wakati wote ulisema utakapoitwa utaitika na utakwenda basi na hilo lipokee kwa imani hiyo wakati Mungu atakapokujalia afya njema. Basi tumepokea ombi lenu na wajibu wenu ni kuniombea na kunipa ushirikiano,” amesema Dk Shoo.
Katika Mkutano huo, Msaidizi wa Askofu, Mchungaji, Deogratius Msanya amechaguliwa kwa kipindi cha pili ambapo katika kura 332 zilizopigwa kura za ndio zilikuwa 324, za hapana ni sita na mbili ziliharibika.
Akizungumzia kuhusuuchaguzi huo, Mchungaji Msanya amewashukuru wajumbe kwa kuonyesha imani kwake na kuwaomba ushirikiano.
“Nawashukuru kwa ushirikiano mlionipa kwa kipindi kilichopita na sasa naomba muendelee kunipa ushirikiano na kwa neema ya Mungu tuendelee kutumika kwa pamoja kumsaidia kiongozi wetu ili kuweza kutekeleza majukumu ambayo Mungu amemuitia katika dayosisi yetu na yote yawe kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu.”