Aziz Ki amwachia Dube kiatu

WAKATI Yanga jana ilikuwa uwanjani kuvaana na Kagera Sugar katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, staa wa timu hiyo Stephane Aziz Ki ameamua kujisalimisha mapema kwa kumtaja mrithi wa kiatu cha Mfungaji Bora akimpa Prince Dube.

Aziz Ki anayeichezea Yanga kwa msimu wa tatu, ndiye Mfungaji Bora wa Ligi msimu uliopita akitupia mabao 21 na kabla ya kuja nchini alishawahi kunyakua kiatu kama hicho katika Ligi Kuu ya Ivory Coast akiwa na ASEC Mimosas.

Kabla ya Aziz Ki, Mfungaji Bora wa Ligi Kuu alikuwa ni Fiston Mayele aliyekuwa nyota wa Yanga pia kisha kutua Pyramids ya Misri sambamba na Saido Ntibazonkiza wa Simba ambaye kwa sasa hayupo ndani ya timu hiyo baada ya kutemwa msimu huu, kila mmoja akimaliza na mabao 17.

Kutokana na mfululizo wa mastaa wa Yanga kunyakua tuzo hiyo, safari hii Aziz Ki aliliambia Mwanaspoti anaona kiatu cha msimu huu kitaenda kwa Dube aliyesajiliwa msimu huu akitokea Azam FC.

Kiungo mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso, alisema msimu uliopita alikuwa na presha kubwa kutokana na mashabiki wa Yanga walikuwa wanataka kuona anakuwa mfungaji bora, japo haikuwa malengo yake, lakini safari hii hataki tena kuishi maisha hayo na anakabidhi usinga kwa Dube na Jean Baleke.

Aziz KI alisema ujio wa washambuliaji hao wapya, yaani Dube na Baleke kumempa utulivu mkubwa kwani anaamini katika uwezo wao kuwa watakwenda kufanya makubwa ukizingatia kuwa kazi yao kubwa ni kufunga na haoni kwa nini Dube asinyakue tuzo hiyo kwa uwezo alionao wa kucheka na nyavu.

“Imani yangu ipo kwa Dube, kwani jamaa anastahili kunipokea tuzo hii. Sio siri msimu uliopita nilikuwa na presha kubwa kutokana na mashabiki wa Yanga kutaka kuona nakuwa mfungaji bora mbele ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ niliyekuwa nachuana naye, japo haikuwa shabaha yangu, nilifanikiwa,” alisema Aziz Ki na kuongeza;

“Kwa kikosi tulichonacho mshambuliaji kama Dube ni rahisi kufunga sana, kwani viungo ni wengi ambao wana uwezo mkubwa wa kumlisha mipira hata katika mechi kadhaa zilizopita nadhani mmeona kilichotokea. Atafunga.”

Msimu uliopita Dube akiwa na Azam akiichezea kwa nusu msimu alifunga mabao saba na kumfanya afikishe jumla ya mabao 33 katika misimu minne kwani alijiunga na timu hiyo mwaka 2020 akitokea Highlanders ya Zimbabwe.

Tangu atue Jangwani, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Zimbabwe, ameshafunga jumla ya mabao matatu yakiwamo mawili ya Ligi ya Mabingwa Afrika na moja la Ngao ya Jamii, mbali na yale ya mechi za kirafiki timu ilipokuwa kambini Afrika Kusini.

Mbali na Dube na Baleke, Yanga pia ina washambuliaji wengine akiwamo Kennedy Musonda aliyefunga mabao matano ya Ligi Kuu na Clement Mzize aliyefunga mabao sita ya Ligi na matano ya Kombe la Shirikisho yaliyompa tuzo ya Mfungaji Bora licha ya kulingana na Edward Songo wa JKT Tanzania.

Related Posts