Badru: Kachwele ni Samatta mtupu

KOCHA mpya wa Songea United, Mohammed Badru amempigia chapuo kijana aliyemnoa katika timu za vijana pale Azam, Cyprian Kachwele ambaye kwa sasa anaichezea Vancouver Whitecaps ya Canada kuwa anaweza kuvaa viatu vya nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta katika kikosi cha Taifa Stars.

Kachwele ni miongoni mwa washambuliaji wanne wa kati akiwemo Wazir Junior na Clement Mzize ambao wameitwa kikosi hicho kwa ajili ya michezo miwili ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za Afcon 2025 dhidi ya Ethiopia na Guinea.

Badru alisema Kachwele ni mshambuliaji wa kati mwenye sifa tatu tofauti akimlinganisha na washambuliaji wengine vijana.

“Samatta ndio anamaliza hivyo nani anafuata inawezekana ndio swali ambalo wadau wengi wamekuwa wakijiuliza, binafsi namwona Kachwele, nimemfundisha najua uwezo wake na nimekuwa nikifuatilia mwenendo wake, ni mshambuliaji mwenye njaa ya kufunga na alionyesha hilo kwenye ligi za vijana,” alisema na kuongeza;

“Kachwele anakupa faida ya kukaa na mpira wakati timu ikisogea juu, ni mzuri katika matumizi ya nafasi lakini pia anaweza kutokea pembeni, kwa umri wake na nafasi ambayo amekuwa akipewa Canada hiyo inaonyesha vile alivyo na kipaji kikubwa ni wakati sasa wa kuanza kumpa nafasi ya kucheza.”

Badru aliendelea kumuongelea kwa kusema wapo washambuliaji wengine vijana ambao wanafanya vizuri mfano Valentino Mashaka wa Simba na hata Mzize lakini wanaweza kupigwa gepu na Kachwele kutokana na levo yake ya ushindani kwani ana njaa ya mabao kama alivyo nahodha huyo wa Stars anayecheza Ugiriki.

“Mwenzao amepata nafasi ya kuonyesha makali yake kwenye moja ya ligi kubwa hivyo uwezo wake wa ushindani lazima tutegemee kuona ukikua zaidi,” alisema Badru.

Related Posts