BSM, safari ya mafanikio, urithi usiofutika MCL

Bakari Steven Machumu (BSM) ameaga MCL akiwa na urithi mkubwa katika uongozi, uandishi wa habari, na ubunifu.
Naam. Rafiki yangu na mwanahabari mwenzangu, Bakari Steven Machumu ambaye anapenda kulifupisha jina lake kwa herufi tatu – BSM, amemaliza safari ya kutukuka kitaaluma, kihabari na kiuongozi katika kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL).

Bakari au BSM kama ninavyopenda kumwita, tangu tukutane katika tasnia ya habari mwaka 1998, anahitimisha safari yake akiwa amefanikiwa kuvuka kwa mafanikio makubwa ngazi takriban zote muhimu za kikazi katika chumba cha habari.

Anaondoka MCL akiwa ameacha alama zisizofutika na urathi (legacy) wa mfano na bora kabisa katika ustawi, kwanza kwake mwenyewe, pili kampuni husika na tatu katika medani ya taaluma ya habari, akiwa pengine ndiye mwanahabari aliyefanikiwa zaidi kikazi kuliko mwingine yeyote nyakati hizi.

Hakuna shaka hata kidogo kwamba, tangu ashike kwanza nafasi ya kuwa Mhariri Mtendaji Mkuu katika MCL na baadaye kuwa Mkurugenzi Mtendaji, BSM alifanikiwa kuipandisha kampuni hiyo na kuwa kinara katika uchapaji wa magazeti.

Taratibu na kwa sababu ya maono ya mbali aliyokuwa nayo akishirikiana na watendaji wenzake, alifanikiwa kuifanya MCL kusimama imara, ikizitoa jasho sokoni kampuni nyngine za magazeti, zikiwamo The Guardian Ltd, The Business Times Ltd, New Habari (2006) Ltd na Free Media Ltd ambayo kwa nyakati tofauti yalikuwa na sauti kubwa na kutikisa ulimwengu wa habari kitaifa.

Wakati akifika MCL mwaka 2004 akitokea Business Times, alinikuta nikiwa nimeshakaa hapo kwa miaka minne na nikiwa mhariri wa gazeti la Mwananchi Jumapili.

Japo alifika hapo akiwa Mhariri wa Biashara wa gazeti la Kingereza la The Citizen na akiwa mdogo kwangu kwa miaka mitatu kuzaliwa, haikutuchukua muda mrefu kujenga urafiki, huku kiungo kikubwa katika ukaribu wetu akiwa ni mhariri mwingine, Dennis Msacky, ambaye tayari yeye na BSM walishakuwa watu wa karibu kwa miaka mingi kabla.

BSM ambaye kwa hulka ni mtu msikilizaji zaidi kuliko msemaji na anaposema ni mwangalifu sana kuchagua maneno ya kusema, taratibu alianza kuaminika na muda mfupi baadaye akawa ndiye Mhariri Mtendaji wa gazeti la The Citizen.

Miaka miwili baada ya kufanya kazi na BSM, niliondoka na kujiunga na kampuni ya Free Media Ltd ambako nilikwenda nikawa Mhariri Mkuu na baadaye Mhariri Mtendaji wake.

Kwa namna isiyoweza kuelezeka, ukaribu wetu kikazi na kifikra uliendelea kuwa mkubwa zaidi, miye nikichota kutoka kwake maarifa ya namna ya kuandika habari za kibiashara huku yeye akivutiwa sana na uchambuzi wangu wa masuala ya kisiasa.

Wakati wote huo, BSM alikuwa haachi kunieleza ukweli kwamba, alikuwa akifuatilia kwa karibu kila nilichokuwa nikiandika kuhusu siasa, uongozi na masuala yanayohusu utawala bora na siku zote angependa kuwa na uelewa na ufahamu mpana zaidi wa mambo hayo.

Ni katika hatua hii ndipo nilipoanza kutambua namna BSM alivyokuwa akifanya juhudi kubwa ya kufuatilia masuala ya siasa kila wakati tulipokaa na nikawa nasikia mara kadhaa akiwa ameandamana na timu ya wahariri wenzake wa MCL kwenye mazungumzo ya ndani na ya wazi na wanasiasa wa kariba tofauti.

Alilifanya hilo wakati huo akiwa karibu zaidi kikazi na rafiki yake Msacky lakini akawa pia anafuatilia pia masuala ya michezo kupitia kwa Frank Sanga ambaye wakati huo alikuwa mhariri wa gazeti bora la michezo MCL la Mwanaspoti.

Ukaribu wa BSM, Msacky na Sanga uliwaweka karibu kikazi na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MCL wakati huo Sam Shollei na watatu hao wakiongozwa na Msacky wakaniunganisha miye pia katika ushirika wa kifikra wa nje ya ofisi.

Mara kadhaa, nilijikuta nikiwa katika mikusanyiko ya kirafiki nikiwa na BSM akiwa na marafiki zake hao watatu wakubwa kikazi na wakati fulani walikaribia kabisa kunirejesha MCL kwenda kuungana nao tena.

Ingawa nilikataa ushawishi huo, kipindi hicho ndicho hasa nilipoanza kutambua uwezo mkubwa wa kuona mambo, kufikiri, kutenda na kubuni wa BSM.

Naweza nikakiri kwamba ilikuwa ni baada tu ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, nilipoanza kuona nyota inayong’ara katika uhariri na zaidi uongozi ya BSM na wala sikushangazwa hata kidogo niliposikia kila wakati akipanda ngazi taratibu ndani ya MCL na zaidi akijijengea heshima kubwa.

Haiba yake ya utulivu na uamuzi wake thabiti wa kubakia MCL, ulianza kumjengea kuaminika zaidi hadi katika viunga vya yaliko makao makuu ya kampuni mama ya MCL ya Nation Media Group (NMG) huko Nairobi.

Kwa nyakati tofauti nikiwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Habari Tanzania (TEF) kati ya mwaka 2010 na 2016, nilipata fursa kadhaa za kusafiri na BSM katika maeneo tofauti nchini na wakati fulani nchini Kenya na Uturuki.

Safari za ndani na za nje ziliimarisha zaidi ukaribu wetu wa kikazi na kitaaluma na kupitia kwake nikawa navuna wingi wa hekima na maarifa yake ya kikazi, ambayo kwa maoni yangu yalichagizwa sana na kile walichokuwa wakijifunza Nairobi na nje ya hapo.

Yalipoanza kutokea mabadiliko makubwa ya kiteknolojia na kihabari, BSM alichukua hatua za haraka kutafuta fursa ya kupata maarifa zaidi ya kitaaluma akajiunga na masomo ya Shahada ya Uzamili ya Biashara katika chuo cha ESAMI.
Alipomaliza elimu yake kwa mafanikio makubwa, nilimuona BSM mpya aliyekuwa na maarifa makubwa zaidi kuliko niliyeanza kumfahamu mwaka 1998.

Wakati wa vuguvugu kubwa la kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, BSM alikuwa mmoja wa wahariri wachache waliokataa kunaswa katika mtego wa kuegemea upande fulani wa wagombea au vyama vya siasa na akahakikisha magazeti ya MCL, hasa Mwananchi na The Citizen yakichukua mrengo wa kihariri wa kutofungamana na upande wowote.

Msimamo huo si tu aliusimamia katika uhariri, maana tayari alishakuwa ndiye Mhariri Mtendaji Mkuu MCL, bali uliendana na hulka yake binafsi akiwa hata nje ya chumba cha habari.

Nidhamu kubwa ya kikazi na usimamizi usioyumba katika maadili ya uandishi wa habari ni mambo yaliyoanza kumpambanua kama kiongozi thabiti aliyetuzidi maarifa marafiki zake kadhaa.

Sambamba na hilo, kwa namna ambayo  pengine ninaweza nikashindwa kueleza, BSM alikuwa mwepesi sana katika kuiongoza kwanza Idara ya Uhariri aliyokuwa akiiongoza katika mabadiliko ya kijiditali, akiendeleza kazi ambayo msingi wake ulianza kujengwa na mtangulizi wake, Theophil Makunga, ambaye wengi wetu, akiwamo BSM tumepita katika malezi na makuzi yake.

Alipoona kasi ya mabadiliko ni kubwa, BSM kwa kushauriana na rafiki yake mwingine mkubwa Sanga, aliamua kujiunga na masomo ya shahada nyingine tena ya Uzamili ya Uongozi katika Vyombo vya Habari na Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Aga Khan, ambayo aliyamaliza akiwa mwanafunzi kinara.

Mwananchi ya leo inayoendeshwa kwa namna yaendeshwavo mashirika makubwa ya kibiashara ya kitaifa na kimataifa kwa kiwango kikubwa ni matokeo ya maono, ushawishi, ubunifu na wepesi wa kujifunza na kuongoza wa BSM.

Related Posts