Hatari za kiafya kulala muda mfupi baada ya kula

Dar es Salaam. Katika maisha ya sasa, watu wengi wana ratiba zilizojaa shughuli nyingi, kiasi kwamba mara nyingi shughuli hizo huwa chanzo cha kurejea nyumbani usiku na kulala muda mfupi baada ya kula chakula.

Hilo linaweza kuonekana kama jambo la kawaida, lakini ni muhimu kuelewa athari zinazoweza kutokea endapo utalala muda mfupi baada ya kula chakula chako.

Wataalamu wa afya nchini Marekani wanasema muda mzuri wa kula chakula cha jioni kwa mtu yeyote ni kati ya dakika 180 (saa tatu) au dakika 240 (saa nne) kabla ya kupanda kitandani kulala. Kwa kufanya hivyo, wanasema kunaupa mwili nafasi ya kufanyia kazi chakula hicho kama inavyotakiwa.

Wataalamu hao wanasema saa tatu au nne kabla ya mtu kulala, ndiyo muda sahihi zaidi kwa kuwa mwili unaweza kukifanyia kazi chakula kama inavyotakiwa ikiwemo mmeng’enyo lakini pia kunamuepusha mtu kukumbana na magonjwa mbalimbali.

Utafiti huu unakazia ripoti ya Julai mwaka 2018 ambayo ilisema watu wanaokula chakula cha jioni kabla ya saa tatu usiku au angalau saa mbili kabla ya kulala wana hatari ya chini ya asilimia 20 kupata saratani ya matiti na kibofu, kuliko wale wanaokula chakula saa nne usiku au wale wanaokwenda kulala muda mfupi baada ya kula chakula.

Ushauri mwingine wa wataalamu umesema kunywa maji baada ya chakula ni muhimu kwa kila mtu. Lakini kila mmoja anapaswa kufanya hivyo angalau dakika 30 baada ya kumaliza kula chakula.

Mwananchi lilizungumza na Akilimali Minja, mkazi wa Kawe Beach kuhusiana na hilo na alisema kwa kawaida, hulala saa moja na nusu baada ya kula chakula cha usiku.

“Jioni baada ya kupata chakula cha usiku huwa natumia saa moja na nusu kukaa na kutazama mambo kadhaa yaliyotokea duniani kipitia mitandao ya kijamii pamoja na kupanga mipango yangu ya siku inayofuata (kesho) kisha nalala,” anasema.

Anasema katika mazingira ya kazi zake, ni ngumu kukaa saa tatu au mbili ndipo alale kwa sababu mara nyingi hurudi nyumbani kwa kuchelewa, hivyo hujitahidi kuvumilia kulala saa moja baada ya kula chakula.

Kwa upande wake Bhoke Marwa, mkazi wa Songea anasema ni ngumu kuvumilia kukaa kwa saa tatu baada ya kula chakula cha usiku kisha alale.

“Kwa kawaida, natoka asubuhi sana kwenda kazini, narudi usiku. Kuna wakati nikitoka kazini mpaka kufika nyumbani huwa natuamia muda mrefu kidogo. Nikifika naanza kupika, naweza nikamaliza saa nne hapo nikisema nikae kwa saa tatu au mbili maana yake nitakuwa nalala saa sita au saba ni suala gumu kwa sababu kesho tena nitatakiwa kuwahi kuamka,” anasema.

Kwa mujibu wa Mtaalamu bingwa wa magonjwa ya moyo, Profesa Mohamed Janabi ni muhimu kuzingatia kupata mlo kabla ya saa moja usiku ili angalau muda mwingi uutumie kufanya mambo mengine kabla ya kwenda kulala.

Anasema kula chakula na kulala ni makosa ambayo hufanywa na wengi na kuhatarisha afya zao bila kujua.

Profesa Janabi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, anasema ni muhimu kuzingatia uzito usizidi kwa kupanga mlo bora na kula pale mtu anaposikia njaa.

“Chakula kingi, kisicho bora na bila kipimo ni chanzo cha vitambi, uzito kupita kiasi ambao huzaa shinikizo la damu ndiyo huzalisha magonjwa ya moyo, ini na baadaye magonjwa ya figo.

“Kitu cha kwanza ni nidhamu ya kula, umekula chakula cha mchana kwa sababu una njaa au unakula tu? Pia zingatia kula mlo wa usiku saa 12 jioni ili unapolala uchakataji uwe umefanyika,” anasema Profesa Janabi.

Anasema ni muhimu kupima afya ya mwili mara kwa mara na kuwa mwangalifu katika kuangalia presha ya damu na mafuta mwilini, kupunguza uwezekano wa kupata kisukari na uzito uliozidi na kufanya mazoezi.

Hata hivyo daktari wa binadamu, Erick Shayo anasema hiyo si tu kwa watu wazima bali hata watoto wanaweza kukumbana na matatizo hayo, hasa katika mazingira ya Kiafrika ambapo huhimizwa kula, kuoga na kwenda kulala ili waweze kupumzika.

“Kuruhusu hili ndipo tunakutana na matokeo ya watoto kutokewa na chakula kwenye pua, kupaliwa na wakati mwingine kutapika kwa sababu hakupewa muda wa kusubiri chakula kimeng’enywe,” alisema.

Pia, alisema ni rahisi kupata kiungulia kutokana na tindikali ya tumboni kuhama kwa njia isiyo sahihi na kulazimisha kurudi kwenye umio, hivyo ili kuzuia hali hii inatakiwa kulala saa tatu baada ya kula.

Mbali na madhara hayo ambayo yanaweza kupatikana endapo mtu atachelewa kula pia yanatajwa magojwa ya kisukari.

Hilo limethibitishwa na Ofisa Lishe Mwandamizi, kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe nchini (TFNC) Adeline Munuo kwa kueleza kuwa usiku mtu anashauriwa kula mapema halafu akae saa walau mbili ndiyo akalale.

Pia anashauri usiku watu kupunguza kula vyakula vya wanga kama wali au ugali, badala yake wajikite kula mboga mboga na matunda.

“Asubuhi unaweza kula chakula kizito kwa sababu mwili utaushughulisha na mazoezi ya kutembea na kufanya kazi nyingine, lakini usiku watu wanakula chakula na kulala.

“Hapo mwili haupati muda wa kufanya mazoezi, hivyo ndiyo maana tunashauri mlo wa usiku uwe mwepesi au kula chakula ambacho kina wanga kwa kiasi kidogo,” anafafanua.

Huku kwa wale waliopo kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari anawataja ni wanaokula kupita kiasi na ambao hawafanyi mazoezi kwa maana ya kutembea na kufanya shughuli nyingine.

Anasema kila mtu anapaswa ale mlo kamili unaohusisha chakula mchanganyiko kutoka katika makundi matano ya chakula bila kusahau kufanya mazoezi hata ya kutembea.

Anayataja makundi hayo kuwa ni kundi la vyakula vya nafaka, viazi, mihogo na ndizi.

Lingine ni kundi la vyakula vya jamii ya kunde na vya asili ya wanyama, matunda, mbogamboga, mafuta na sukari.

Licha ya kuwa athari hizi zinaweza kutokea kwa jami lakini inaonekana bado haina elimu juu ya ulaji sahihi wa chakula hasa kwa wakati wa usiku.

Related Posts