MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Raia wa Marekani, Brandon Dashaurn Summerlin kutumikia kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Mescaline zenye uzito wa gramu 56.04.
Pia imeamuru kielelezo ambacho ni gramu 56.04 za dawa za kulevya aina ya Mescaline kiharibiwe kwa mujibu wa sheria ya dawa za kulevya
Hukumu hiyo imesomwa Agosti 29,2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Fahamu Kibona ambaye amesema mahakama imeridhika na ushahidi wa mashahidi 9 wa upande wa mashtaka waliofika mahakamani hapo kutoa ushahidi wao dhidi ya mshtakiwa na vielelezo saba vilivyotolewa katika kuthibitisha mashtaka.
Mapema,ilielezwa kuwa, Novemba 12, 2022 huko Posta ndani ya Wilaya ya Ilala Mkoani Dar es Salaam, maafisa wa mamlaka ya kuthibiti na kupambana na dawa za kulevya walimkamata mshtakiwa akiwa anachukua kifurushi chenye dawa hizo ambazo aliziagiza kutoka nchini Peru.
Kufuatia kukamatwa kwake, mshtakiwa Brandon alifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Mescaline.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Kibona amesema, upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mtuhumiwa alitenda kosa.
Hata hivyo kabla ya kusomwa kwa adhabu hiyo, mahakama iliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema ndipo wakili wa Serikali Titus Aron alidai hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya mshtakiwa ila waliomba apewe adhabu kali.
“Mheshimiwa tunaomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wale ambao wanafanya biashara hii na wale wenye mpango wa kujiingiza katika biashara hii.
“Mheshimiwa Hakimu madhara ya dawa za kulevya kama yalivyoelezwa katika taarifa ya Mkemia yanasababisha ulevi usioponyeka, kuharibikiwa kwa akili na pia ni dawa zilizopo kwenye kundi la sumu athari ambazo ni mbaya na zenye madhara makubwa kwenye afya ya binadamu…., pia dawa hizi zinaharibu akili ya vijana ambao ni nguvu kazi katika ukuaji wa uchumi kijamii.” Amesema Aron
Kwa upande wake mshtakiwa ambaye aliwakilishwa na wakili Faith Mwakoti lakini alijitetea mwenyewe ameiambia mahakama kuwa alikuwa akitumia dawa hizo kama kiburudisho cha kuweza kumsaidia ‘kurelax’.
Mshtakiwa alipoulizwa maombi yake dhidi ya shtaka linalmkabili aliiambia mahakama kuwa ifanye inavyoona inafaa katika kutoa adhabu (let the court do as it pleases).
“Mahakama imezingatia maoni ya upande wa mashtaka kuhusu athari za dawa za kulevya kiafya kijamii, kiuchumi na kimataifa na utetezi wa mshtakiwa, na hivyo baada ya kuzingatia maoni ya pande zote mbili mahakama inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 30 gerezani”. Amesema hakimu Kibona. Haki ya kukata rufaa kwa mshtakiwa iko wazi.