Na Imani Nathaniel, Mtanzania Digital
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeahirisha kesi ya tuhuma ya kujeruhi na kutoa lugha chafu inayomkabili wanandoa Bharat Nathwan (57), Sangita Bharat (54) hadi Septemba 10, 2024 kwa sababu ya kutokuwepo kwa wakili wa washtakiwa kwa taarifa kwamba yupo Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.
Wanandoa hao ambao wanaoishi Mtaa wa Mrima – Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashtaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.
Taarifa hiyo imetolewa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Ngukah mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya wa mahakama hiyo, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka.
Wakili Ngukah alidai kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa na walikuwa na mashahidi wawili, lakini wamepokea barua kutoka kwa Wakili wa utetezi Edward Chuwa kwamba ana kesi Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.
“Yupo kwenye kesi namba 19857/2024 kati ya Agustino Kavishe dhidi ya William Kideme na wengine mbele ya Jaji Hemed, barua hii iliambatanishwa na chamber summons”alidai Wakili Ngukah
Alidai kuwa kutokana na sababu hiyo, wanaomba wapangiwe tarehe nyingine, Wakili Chuwa amependekeza kwamba iwe Septemba 10, mwaka huu.
Hakimu Lyamuya baada ya kusikiliza taarifa hiyo, alisema kuwa na wao walipata barua hiyo juzi, anawaonya mashahidi hao waliyokuwa mbele ya mahakama wafike mahakamani Septemba 10,2024 kwa ajili ya kutoa ushahidi wao.
Ilidaiwa kuwa Nathwan anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.