Kesi ya wakulima wa miwa dhidi ya Waziri wa Kilimo, kuunguruma mwezi ujao

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ya Dar es Salaam, imepanga Septemba 18, 2024 kuanza kusikiliza kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na George Mzigowandevu na wenzake 23, dhidi ya Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

George na wenzake 23 kwa niaba ya wakulima wenzao 11,000 wa miwa kutoka Bonde la Kilombero, wamefungua kesi hiyo mahakamani hapo wakipinga kuondolewa kwa kinga ya uingizwaji wa sukari baada ya kufanyika mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Kesi hiyo ilipangwa leo mbele ya Jaji Dk Angelo Rumisha, kwa ajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuanza usikilizwaji.

Katika malalamiko hayo, wakulima hao wanadai kifungu hicho kinabadili Mamlaka ya kuagiza sukari ya akiba kutoka kwa wazalishaji ambao wakati wa uongozi uliopita, ziliagizwa zifanye na kampuni ya uzalishaji sukari ya wazalendo wa Tanzania

Pia, wakipinga uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.

Mzigowandevu pamoja na mambo mengine anadaiwa kuwa mabadiliko hayo yanaipa mamlaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ya uagizaji wa sukari.

Alidai kuwa kitendo hicho kitazuia au kitafanya ugumu wa mazao yao ya miwa kutouzika katika viwanda vya miwa.

Leo kesi hiyo ilipotajwa Mzigowandevu na wenzake waliwakilishwa na jopo la mawakili sita wakiongoza na wakili Mwandamizi wa utetezi Mpare Mpoki akishirikiana na Dk Rugemeleza Nshala, Rais mstaafu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Wengine ni John Seka ambaye pia ni rais mstaafu wa TLS, rais wa sasa wa TLS, Boniface Mwabukusi, Ferdinand Makore na Edson Kilatu na Paul Kisabo

Kwa upande wa wajibu maombi ambao ni Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inaliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a akishirikiana na wakili wa Serikali Mwandamizi, Jacqline Kinyasi.

Chang’a alidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba wamepewa nyaraka kwa waleta maombi Agosti 27, 2024 hivyo wanaomba wapewe siku 14 ili waweze kujibu madai hayo.

Chang’a baada ya kueleza hayo, Wakili Mpoki alidai hawana pingamizi juu ya wajibu maombi kupewa siku 14 na kwamba huo ni utaratibu kisheria.

Jaji Dk Rumisha baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 18, 2024 saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya usikilizaji.

Hata hivyo waleta maombi hao 24 walikuwepo mahakamani hapo wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Pia, shauri hilo lilisikilizwa kwa njia ya video huku waleta maombi na wajibu maombi wakiwa mahakamani, huku jaji akitumia luninga iliyofungwa mifumo ya Tehama kuongea na mawakili hao pamoja na wakulima waliofungua shauri hilo.

Related Posts