Kukosa maji siku mbili kulivyozua kizaazaa Dar, Dawasco yafafanua

Dar es Salaam. Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani wameeleza kero walizopata kwa kukosa maji kwa siku mbili mfululizo, huku wakilalamika kuwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Dawasa) kuwa imechelewa kutoa taarifa za tatizo hilo.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Dawasa, Everlasting Lyaro amesema kulikuwa na hitilafu ya umeme katika mtambo wa Ruvu Juu, tatizo ambalo lilichukua saa 18 kurekebishwa.

Ameongeza kuwa matengenezo yamekamilika leo asubuhi na mtambo umeanza kufanya kazi tena.

“Tunategemea maji yatarudi kwa baadhi ya maeneo, lakini itachukua zaidi ya siku moja hadi msukumo wa maji uwe sawa kwa sababu mabomba hayakuwa na maji,” amesema Lyaro.

Ufafanuzi huo umetokana na malalamiko ya baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi leo Agosti 30, 2024, kuwa maji bado hayajafika maeneo yao, huku wengine wakidai kuwa yalirudi kuanzia saa nane usiku.

Jacob Harrison, mkazi wa Kimara, amesema hana utaratibu wa kuhifadhi maji kwa kuwa eneo lake halina kawaida ya huduma hiyo kukatika, lakini sasa ana siku ya tano bila maji na hakuwa na taarifa ya ukatikaji huo.

“Imenibidi kununua maji kwa siku hizi kadhaa. Nimetumia Sh7,000 kwa sababu nina familia ya watu watano na mtoto mdogo, hivyo nimejikuta natumia gharama kubwa ya maji,” amesema Jacob.

Hali iko hivyo kwa Japhary Hamad, mkazi wa Kibaha, ambaye amesema tangazo la Dawasa limetolewa baada ya wao kukosa maji kwa takribani siku nne, na kuwa imekuwa kawaida maji kukatika kwa zaidi ya siku mbili na kurudi usiku wa manane.

“Tumeanza kuzoea mazingira ya kukosa maji. Ni siku ya tano sasa na watoto wanaenda shule, na sisi wengine tuna shughuli zetu. Tumelazimika kuiona hali hii kama ya kawaida ingawa tunapata shida,” amesema Japhary.

Lakini Halima Yahya, mkazi wa Tabata, yeye amesema wamekuwa wakitumia maji ya kisima yenye chumvi kwa kuwa hawajui yale ya Dawasa yatatoka lini na muda gani.

“Hapa ninapoishi kuna kisima lakini ni maji ya chumvi. Tunatumia kwa ajili ya chooni na kupigia deki, lakini kwa mambo mengine tuna wakati mgumu, hasa kwenye kuoga. Tunaharibu ngozi zetu na wakati mwingine watu wanapauka,” amesema Halima.

Maeneo yanayotajwa kuathiriwa na ukosefu wa maji ni pamoja na Mlandizi, Msufini, Vigwaza, Chamakweza, Ruvu, Kwa Mathias, Pangani Bokomnemela, Kibaha, Visiga, Picha ya Ndege.

Maeneo mengine yaliyokumbwa na kadhia hiyo ni Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Makabe, Kimara, Msewe, Changanyikeni, Mabibo, Kisarawe, Ukonga, Kinyerezi, Tabata, Temeke, Segerea, Makuburi, Ubungo Maziwa, Tabata Relini, Kiwalani, Lumo, na Yombo Vituka.

Pia maeneo ya Uwanja wa Ndege, Banana, Viwanda vya Barabara ya Nyerere, Jet, Buguruni na Tazara nayo yameathirika.

Related Posts