Moshi. Wakazi zaidi ya 15,800 wa Kata ya Mbokomu, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ambao walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji safi baada ya miundombinu ya huduma hiyo kusombwa na mafuriko Mei 2024, wanatarajia kuondokana na adha hiyo kuanzia Jumatatu, Septemba 2, 2024.
Kata hiyo, yenye vijiji vitatu vya Korini Kusini, Korini Kati, na Korini Juu, inahudumiwa na maji safi kutoka katika chanzo cha Mrusunga.
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) imeanza matengenezo na maboresho ya miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko hayo.
Mwananchi alitembelea eneo hilo na kushuhudia mafundi wakiendelea na ukarabati, kusafisha chanzo hicho na kurejesha mabomba yaliyoharibiwa.
Akizungumza baada ya kukagua maboresho hayo leo, Agosti 30, 2024, Mhandisi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji Safi wa Muwsa, Deogratius Lyimo amesema wanaendelea na ukarabati na ifikapo Septemba 2, 2024, huduma ya maji itarejea katika Kata ya Mbokomu kama kawaida.
Amesema kwa sasa wananchi wanapata maji kwa mgao kupitia vituo 18 vya kutolea huduma (vilula) kutoka katika vyanzo vya Lucy Lameck na West.
“Tumesafisha kwa asilimia 70 ndani ya chanzo, na sasa tunaendelea kuondoa takataka zote nje ya chanzo na kurejesha mabomba. Tunatarajia kukamilisha kazi hii Septemba 2, 2024, kama maelekezo yalivyotolewa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso,” amesema.
Amesema mahitaji ya maji katika Kata ya Mbokomu ni mita za ujazo 1,110, na chanzo hicho kinazalisha mita za ujazo 1,200 hadi 1,300 kwa siku, na hivyo amewaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu wakati ukarabati unaendelea.
Akizungumzia uharibifu uliosababishwa na mafuriko hayo, Lyimo amesema chanzo hicho cha maji, kilijaa magogo, mchanga, na mawe, huku mabomba yenye urefu wa mita 700 yakisombwa na mafuriko.
Diwani wa Kata ya Mbokomu, Raphael Materu, ameishukuru Muwsa kwa kuchukua hatua za haraka kurejesha miundombinu hiyo ya maji, kwani wananchi walikuwa wakitaabika kwa muda mrefu.
“Tunaishukuru Muwsa kwa kutenga fedha zake za mapato ya ndani na kuanza ukarabati kwa ajili ya kurejesha chanzo hicho ambacho miundombinu yake iliharibiwa. Ni hatua kubwa na wametuahidi ifikapo Septemba 2, huduma ya maji itarejea,” amesema diwani huyo.