MSIMU uliopita, ungemwambia shabiki wa Simba kwamba mabosi wa klabu yake watamuacha kiungo wao Fabrice Ngoma wangeweza kukutia ngumi achilia mbali kung’aka kwa mshtuko.
Lakini mechi mbili tu ndani ya msimu mpya ukiongeza na zile dakika 45 alizocheza katika Simba Day, zimetosha kumuibua mfalme mpya wa eneo la kiungo cha ulinzi, Debora Fernandes Mavambo. Huwaambii kitu mashabiki kuhusu mtu huyu.
Ndani ya dakika 180 alizocheza katika mechi mbili za Ligi, Mavambo amekata kwa haraka kiu ya mashabiki wa Simba juu ya kupata mtu wa maana anayeweza kuziba kwa usahihi eneo la kiungo wa chini na kuwasahaulisha kuhusu Ngoma.
Simba imehaha kwa muda mrefu kupata kiungo wa aina ya Mavambo ambapo msako huo haukuwa na mafanikio kabla ya sasa kuibuka mzaliwa huyu wa Angola akiwa na asili ya DR Congo ambaye kazi yake imewakosha mashabiki.
Mavambo, moja ya vitu bora vya kwanza anavyoonyesha uwanjani ni uwezo wake wa kukaba kwa nguvu na kuanzisha mashambulizi haraka.
Amekuwa akihaha kila eneo kuhakikisha mpira unaokuja eneo la kati unakuwa katika umiliki ya Simba.
Ulinzi anaoutoa kwa kuziba njia za wapinzani kuifikia ngome ya wekundu hao, umechangia kuifanya timu hiyo kuanza msimu kibabe ikiwa haijaruhusu bao hata moja katika mechi mbili za kwanza huku yenyewe ikifunga mabao 7.
Hii ni mara ya kwanza kwa Simba ndani ya misimu 10 kushinda mechi zote mbili za kwanza kwa ushindi mkubwa wa mabao 7 na bila ya kuruhusu nyavu zao kutingishwa. Msimu ya 2017-18, Simba ilifunga jumla ya mabao 7 katika mechi mbili lakini haikushinda mechi zote mbili za kwanza kwani ya awali ilishinda 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting na iliyofuata ikatoka 0-0 dhidi ya Azam FC.
Jambo la kuvutia pia ni kwamba katika msimu huo ambao Simba ilifunga mabao 7 ndani ya mechi mbili za kwanza, ndio ambao pia ilienda kulirejesha taji la Ligi Kuu Bara ambalo lilikuwa limeshikiliwa na Yanga kwa misimu mitatu mfululizo kama ilivyo sasa. Je, na msimu huu itarudisha taji la ligi kama msimu ule wa 2017-18? Ni jambo la kusubiri.
Mavambo kwa jina rahisi la kisasa wanamuita kiungo wa ‘boksi to boksi’ yaani sekunde moja anaokoa noma kwenye boksi la timu yake na sekunde chache zinazofuata utamkuta analeta noma kwenye boksi la wapinzani.
Uwezo huu sio kila kiungo anakuwa nao ndio maana ikawa rahisi kuona anafunga bao kali kwenye ile mechi ya Simba Day lakini pia hata hizi mechi mbili za ligi amefanya majaribio makubwa ya kutafuta mabao.
Kiungo huyu kitu kingine muhimu kitakachompa faida ni umbo lake la kazi na pia urefu wake wa mita 1.78, hapa amekuwa akipata urahisi wa kupambania mipira ya juu lakini pia hata ukitaka kupambana naye kwa nguvu tayari yuko imara akiwa ameshiba vizuri kimazoezi.
Kama unacheza na Simba basi wachezaji wako wanatakiwa kuhakikisha wanapomuona Mavambo amepanda juu basi wanatakiwa kuwa makini kuhakikisha ile mipira ya pili au hata akisogea kwa kupandisha mashambulizi wasimpe nafasi ya kujaribu, kutokana na shabaha yake.
Mavambo pia ukiachana mashuti lakini pia amekuwea na uthubutu wa kushambulia kwa vichwa katika mashambulizi ya kona na hata mapigo ya adhabu ndogo ingawa bado hajafanikiwa kufunga.
Pale Simba sasa kinachofanyika ni viungo wengine kupambana kuhakikisha nani anachukua nafasi ya kucheza na Mavambo, kwani jamaa kwa ubora anaoendelea kuuonyesha tayari ameshajipata kwa kuingia katika kikosi cha kwanza.
Kama umezingatia namna kocha Fadlu Davids anavyopanga kikosi chake tayari Mavambo yupo ndani ya hesabu zake na kinachofanyika sasa ni kutafutwa kina Mzamiru Yassin, Augustine Okejepha, Yusuf Kagoma na wengine kuangalia nani atacheza naye.
Msimu uliopita kiungo Fabrice Ngoma alikuwa ndio kila kitu pale kati lakini ujio wa Mavambo umebadili kila kitu.
Ngoma amepoteza nafasi ndani ya kikosi hicho cha Simba na kukosekana kwake kikosini hakuwashtui mashabiki, kwa kuangalia mechi hizi chache za kwanza.
Kasi ya Mavambo katika kukaba na kuanzisha mashambulizi inamtofautisha kabisa na Ngoma ambaye licha ya ukali wa kupiga pasi zenye macho, lakini yuko ‘slow’ sana.
Hapa sio Ngoma tu, ilikuwa sahihi kwa Simba kuachana na Babacar Sarr ambaye mapema tu alichaniwa mkataba wake na kushushwa Mavambo na Yusuph Kagoma.
Simba iliwahi kuwa na kiungo bora kama Mavambo, Mkenya Hillary Echesa ambaye alikuwa na ubora kama huo ila anachozidiwa na Muangola huyu ni kasi yake.
Kocha Fadlu amesema bado anaendelea kuitengeneza timu yake na Mavambo ni mmoja kati ya viungo bora ambao anaamini wataibeba timu yake msimu huu.
“Huwa sipendi sana kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja lakini, huyu (Mavambo) ni mmoja kati ya viungo bora nilionao hapa Simba na anaendelea kuimarika.”