Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Makame Machano Hajj, ameeleza umuhimu wa kuimarisha ukaguzi wa vyombo vya majini kwa usalama wa baharini na kupigia debe nchi wanachama wa Hati ya Makubaliano ya Ukaguzi wa Meli katika Bahari ya Hindi (IOMOU) kuongeza juhudi katika ukaguzi.
Katika hotuba yake ya kufunga Mkutano wa 27 wa kimataifa wa IOMOU ulionza Agosti 26 na kuhitimishwa Agosti 30, 2024, Hajji ameeleza kuwa licha ya Tanzania kutokufanya vizuri katika ukaguzi wa meli kwa miaka mitatu iliyopita, juhudi mpya za kutoa mafunzo kwa wataalamu wa ukaguzi zimezaa matunda.
Amesema mwaka huu, Tanzania imepiga hatua kubwa, ikikagua zaidi ya vyombo vya majini 300, na kupata pongezi kwa kuboresha hali ya ukaguzi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Hati ya IOMOU, Gqabu Tobela, amethibitisha kwamba Tanzania kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) imefanya juhudi kubwa, ikikagua meli 355 mwaka 2023.
Amesema Tanzania imeweza kuvuka malengo kwa ukaguzi wa asilimia 98 ya meli zenye sifa, kulinganisha na asilimia 10 inayotakiwa.
Meneja Usajili na Ukaguzi wa Meli, Said Kaheneko, amesisitiza kwamba kuongeza idadi ya meli zinazokaguliwa ni muhimu kwa usalama wa watu, mizigo na mazingira ya baharini na kusaidia kuepusha ajali zinazotokana na mapungufu ya meli.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Nahason Sigalla, amesema kuimarisha usalama wa majini ni muhimu kwa uchumi, maisha ya watu na kulinda bahari dhidi ya athari zinazoweza kutokea kutokana na meli. Amesema Tanzania imetajwa kama nchi iliyofanya vizuri katika ukaguzi wa meli.
Katibu wa IOMOU, Achintya Dutta, ametoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano na kwa kuadhimisha miaka 25 ya utekelezaji wa IOMOU.
Amesema Tanzania ni mojawapo ya nchi sita za mwanzo zinazoshiriki katika mkataba huu, ambao sasa umeungwa mkono na zaidi ya nchi 20.
IOMOU inalenga kubaini na kutokomeza meli zilizo chini ya kiwango katika Bahari ya Hindi.