Arusha. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amezitaka taasisi na mashirika ya umma kufanya utafiti wa kutosha kuhusu sekta wanazotaka kuwekeza nje ya nchi, kabla ya kufanya uamuzi wa kufanya hivyo.
Pia, amesisitiza kuwa utafiti huo ulengwe juu ya sheria, kanuni, taratibu na sera za nchi wanazotaka kuwekeza ili kuepuka migongano ya kimasilahi na kuepusha hasara ya fedha za umma.
Nsekela amebainisha hayo Agosti 29, 2024, wakati akiwasilisha mada kwenye kikao kazi cha pili cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma, chenye kaulimbiu isemayo “Mikakati ya taasisi na mashirika ya umma kuwekeza nje ya Tanzania.”
Amesema changamoto kubwa ya uwekezaji nje ya nchi ni tofauti za sheria, sera, lugha, na mwenendo wa huduma, hivyo utafiti wa kina unahitajika ili kukabiliana na hayo kabla ya kuwekeza.
Ameeleza kuwa benki yake inatoa elimu hiyo kama moja ya taasisi zilizofanikiwa kuanzisha matawi katika nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), jambo ambalo halikuwa rahisi kulifanikisha.
Amesema benki hiyo sasa ina mpango wa kufikia nchi tano ndani ya miaka minne ijayo.
“Tulipata changamoto hizo, lakini tumefanikiwa. Kikubwa ni taasisi kuwa na uongozi imara na kufanya utafiti wa kutosha kuhusu mnachotaka kuwekeza na mahali uhitaji ulipo. Sisi kama wazoefu tuko tayari kuwasaidia,” amesema Nsekela.
Awali, Waziri wa zamani, Dk Harrison Mwakyembe aliipongeza CRDB kwa uwekezaji wenye mafanikio na kuisihi Serikali kuweka viongozi imara kwenye taasisi za umma, ambao watakuwa na uamuzi wa mafanikio katika sekta zao, badala ya kuwa na hofu ya kuondolewa madarakani mara kwa mara.
“Hapo umezugumzia uongozi imara, hivyo Serikali yetu ione namna ya kuweka viongozi thabiti kwenye hizi taasisi kwa kupitia barua za maombi na wasifu, lakini pia kueleza malengo watakayozifanyia taasisi,” amesema Mwakyembe.
Mwakyembe ameongeza kuwa utaratibu wa sasa wa viongozi wa hizi taasisi kuteuliwa kuongoza taasisi za umma umekuwa chanzo cha mabadiliko ya mara kwa mara kwa kuenguliwa kutokana na baadhi yao kushindwa kuendana na kasi ya kiutendaji inayotakiwa na Rais Dk Samia Suluhu.
Mwanasiasa mkongowe, Stephen Wasira ameitaka benki hiyo kupunguza masharti ya mikopo hasa kwa vijana wanaoanza uwekezaji bila kuwa na mali za dhamana, ili nao waweze kunufaika na taasisi hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dk Athumani Kihamia amesema uwezekano wa taasisi za umma kuwekeza nje upo, lakini changamoto ndogondogo zimekuwa zikizikumba baadhi ya taasisi, ikiwemo mitaji midogo na ukosefu wa uzoefu.
“Zipo faida kubwa za kuwekeza nje, mbali na kuitanua nchi kiuchumi, pia inaongeza ajira kwa watu na soko. Tunaishukuru Serikali yetu kwa kutaka kuja na mfuko wa uwekezaji ambao tunaamini utaleta manufaa makubwa kwa wadau wa sekta za umma,” amesema Dk Kihamia.