Raslimali fedha, woga vyatajwa kukosekana habari za uchunguzi

Dar es Salaam. Wanazuoni wa uandishi wa habari wamejadili changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa uandishi wa habari za uchunguzi, wakitaja mambo mawili kama kikwazo.

Wamesema uandishi wa aina hii unakabiliwa na woga na ukosefu wa fedha, hali inayosababisha waandishi wengi kuacha kuandika habari zenye manufaa kwa jamii na badala yake kufuata masilahi binafsi.

Wamebainisha hayo katika siku ya tatu ya Kongamano la 14 la Jumuiya ya Wadau wa Habari Afrika Mashariki (EACA), leo Agosti 30, 2024.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Dk Samwilu Mwaffisi amesema vyombo vya habari vingi nchini havina uwezo wa kifedha kuwekeza katika uandishi wa uchunguzi, na hivyo waandishi wanajikuta wakiepuka habari zenye mgogoro ili kuepuka migogoro na mamlaka, ikiwemo Serikali.

Dk Mwaffisi amesisitiza kuwa uandishi wa habari ni huduma kwa jamii, lakini sasa umekuwa biashara.

Odette Mpungirehe kutoka Chuo Kikuu cha Rwanda, ameeleza kuwa habari za uchunguzi zina uwezo wa kufichua maisha halisi ya watu wa hali ya chini na kurekebisha makosa katika jamii.

Hata hivyo, ameshauri waandishi wawezeshwe kifedha, kitaaluma na kisheria ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Loth Makuza, mwanzilishi na rais wa zamani wa Chama cha Maofisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST), amekosoa vyombo vya habari kwa kugeuza uandishi kuwa biashara, akisisitiza umuhimu wa uwezeshwaji wa vyombo hivyo ili viweze kufanya kazi ipasavyo na kwa ufanisi.

Dk Mona Mwakalinga, Amidi wa Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, amebainisha kuwa woga umekuwa kikwazo kikubwa kwa waandishi kufanya habari za uchunguzi, akisisitiza kuwa uandishi huo ni muhimu kwa kuwawajibisha wale walio madarakani.

Mwandishi mkongwe Jenerali Ulimwengu ameweka msisitizo kwenye uwajibikaji wa mamlaka akisema vyombo vya habari vina jukumu la kuwawajibisha wale walioko madarakani, badala ya kuwasifia tu.

Kongamano hilo, lililofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), limewakutanisha watafiti, wanazuoni, wahadhiri, wanafunzi, na wataalamu wa sekta ya habari kutoka nchi 25.

Related Posts