Simulizi ya aliyeachiwa huru kesi ya Milembe, wenzake wakihukumiwa kunyongwa

Geita. Musa Pastory (34), Mkazi wa Kijiji cha Buyanga, Kata ya Bugalama, Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga ni kati ya washtakiwa wanne walioshtakiwa wakidaiwa kumuua Milembe Suleiman aliyekuwa mfanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu Geita (GGML).

Agosti 27, 2024, siku ya hukumu ya kesi hiyo wenzake watatu, Dayfath Maunga, Safari Lubingo na Genja Deus walihukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Akizungumza na Mwananchi, hivi karibuni uso ukiwa umejaa tabasamu, anasema yeye kwake ilikuwa siku ya muujiza na matumaini mapya ya maisha baada ya kuachiwa huru.

Musa ni mtoto wa tatu kati ya tisa wa mzee Ally Pastor, mzaliwa wa Kijiji cha Bugalama, ambaye alianza elimu ya msingi Izumba katika Kata ya Lunguya, Kahama.

Anasema akiwa darasa la tano alivushwa na kuingia la saba kutokana na uwezo wake darasani. Baada ya kumaliza darasa la saba alijiunga na Shule ya Sekondari Lunguya.

Anasema juhudi za kusoma, kusikiliza walimu na nidhamu vilimwezesha kufaulu mtihani wa kidato cha nne, hivyo akachaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Bihawana iliyoko mkoani Dodoma.

Mwaka 2014 anasema alichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino tawi la Tabora na alihitimu mwaka 2017 Shahada ya kwanza ya ualimu.

Anasema hakupata ajira kwa elimu aliyosomea, hivyo aliajiriwa katika Mgodi wa Bulyanhulu kitengo cha ulinzi. Mwaka 2021 alioa na aliwajalia mtoto wa kike, hivyo waliendelea na maisha Kakola.

Pastory anasema siku aliyokamatwa alikuwa ametoka kuomba ajira kupitia mtandao baada ya Serikali kutoa tangazo la kuajiri walimu.

Anasema alirudi nyumbani na baadaye jioni alitoka kwenda ‘senta’ eneo ambalo huwa na shughuli nyingi za kijamii. Akiwa hapo anasema walifika wanaume wawili mmoja akiwa na daftari.

Mmoja kati ya hao aliuliza kuhusu mmiliki wa mashine ya kusaga, lakini aliye na daftari alimkazia macho.

“Aliniangalia sana, kwa kuwa sikuwa na kitu sikujali. Baadaye alikuja mwingine mnene, ghafla nikavamiwa wakasema ndio huyu hapa,” anasema.

“Tuliokuwa nao wakaanza kupiga kelele wakitaka kujua kwa nini nimekamatwa. Wakajitambulisha wao ni askari wakaagiza tulale chini, sikubisha nililala maana walinikamata mimi na mtoto wa dada yangu. Lilikuja Land Cruiser gari kama la mgodini, waliokuwa ndani watatu walikuwa wamevaa reflector (kiakisi mwanga) wakashuka wakatuchukua na kutuingiza ndani ya gari,” amesema.

Ndani ya gari anasema walimkuta mwanamume mwingine amekaa chini akiwa na pingu, ambaye alikuwa akilia. Anaeleza walifikishwa Kituo cha Polisi Nyarugusu wilayani Geita.

Anasema walihojiwa na wakiwa mahabusu aligundua katika kesi inayomkabili wako watuhumiwa wengine 14 na kadri walivyohojiwa waliendelea kupungua hadi kubaki sita na mwisho walibaki wanne.

Pastory anasema jambo kubwa alilojifunza katika mchakato wa kesi hiyo ni kuwa, wakati Serikali inafanya kazi unapaswa uiache ifanye, usiingize ugumu kwa kuwa unaposababisha mazingira yawe magumu unaweza kuumizwa.

“Nilichogundua polisi haliwezi kukukamata tu bila kuwa na taarifa zako iwe umefanya kosa au hujafanya lakini lazima kuna mawasiliano yanayowafanya wakufikie, na wanapokufikia wape ushirikiano ukileta ubishi ndiyo hapo unaweza kuumizwa,” anasema.

Anasema wakati wote alitoa ushirikiano wa alichokuwa anajua bila usumbufu.

Pastory anasema kama ilivyo eneo lenye mkusanyiko wa wengi hawakosekani wabaya, ndivyo ilivyo pia kwa Jeshi la Polisi wapo walio wema lakini wapo pia wanaokwenda kinyume cha matakwa ya kazi zao ambao husababisha lilalamikiwe.

“Suala la ukamataji Polisi hulaumiwa, lakini nimejifunza ukikamatwa ujue kuna taarifa zinakusogeza karibu na tukio husika hata kama hujahusika lakini unaweza kuwa umewasiliana na mhalifu hata kama hujui kama yeye ni mhalifu. Kwenye dunia hii ya teknolojia mawasiliano hayafichiki,” amesema.

Tofauti na alivyokuwa akisikia akiwa uraiani, anasema alijua gereza ni sehemu ya jehanamu, eneo linalotisha na lenye mateso lakini kwa muda wa mwaka mmoja aliokaa ndani amegundua ni maneno yasiyo na ukweli.

Musa Pastory (kushoto aliyevaa koti) aliyeachiwa huru katika kesi ya mauaji ya Milembe Suleiman iliyokuwa ikimkabili na wenzake watatu. Katika kesi hiyo wenzake watatu walihukumiwa kunyongwa.

Anasema gereza hasa la Geita ni eneo linalozingatia haki za binadamu na kuwa licha ya kuishi mtindo wa maisha ya gerezani lakini kulikuwa na mazingira bora na haki ya mtu iliheshimiwa.

“Mimi ni mtu mwenye nidhamu tangu nimeanza shule ya msingi hadi chuo kikuu sijawahi kupewa adhabu yoyote ya makosa au utundu, namheshimu yeyote, kabla ya kufika gerezani nilikuwa nasikia mengi wanasema kubaya, unalala chini unapigwa lakini mimi nimekuta tofauti, haki zinasimamiwa.

“Nikiulizwa sekta gani inaongoza kwa kuzingatia haki za binadamu nitasema ni Jeshi la Magereza, ni wasikilizaji na watekelezaji wana roho nzuri,” amesema.

Anasema kama zilivyo sehemu nyingine pia magereza zipo sheria ndogondogo zinazowaongoza na anayeshindwa kuheshimu sheria hizo hupata adhabu lakini siyo kandamizi kama zinavyosemwa mtaani.

“Ukifuata misingi iliyowekwa hakuna anayekugusa. Nimekaa magereza kuanzia Mei 24, 2023 nimetoka Agosti 27, 2024 hakuna siku niliyopigwa, chakula kipo unakula unashiba na hakuna kugombania,” anasema.

Anasema tangu kuanza kesi Mei 24, 2023 katika Mahakama ya Wilaya Geita alijipa tumaini akiamini ipo siku itaisha na haki itatendeka.

“Nilijipa moyo, naamini kutuhumiwa hakukuanzia kwangu na hakutaishia kwangu. Mimi ni raia, wapo waliokamatwa na wakafungwa lakini wapo waliokamatwa na wakaachiwa, hivyo nilikuwa najipa matumani maana nilikuwa na uhakika sijafanya kosa kama haki ipo basi na mimi nitapata haki,” anasema.

Anaeleza kila asubuhi alikuwa anasali akiomba haki itendeke. “Unaomba lakini kwa kuwa umeshaathirika kisaikolojia kuna wakati unashindwa hata kujua ufanye nini.”

“Ni siku isiyosahaulika maishani mwangu ni sawa na suala aliyekamatwa na simba tayari meno mgongoni lakini simba akaamua kuacha kumla. Nilikuwa nimeathirika kisaikolojia japo nilikuwa nimesimama, lakini mwili haukuwa na nguvu roho ilikuwa na matumaini lakini mwili ulikuwa umegoma kidogo nianguke.

“Kisaikolojia sikuwa sawa, nilikuwa nimeharibika mimi si mtaalamu wa sheria japo nilikuwa na uhakika  sijafanya kosa lakini niliona hii ni kama vita iko mbele yangu na lolote linaweza kutokea, nilimuomba Mwenyezi Mungu na kuamini litakalotokea basi ni sawa. Niliamini hata nikifungwa si mimi wa kwanza, kifupi haikuwa rahisi,” anasema.

Picha za watuhumiwa wakiangalia hukumu, umati wa watu, na nyuso za wasikilizaji zilikuwa sehemu ya muktadha wa hukumu hiyo.

Anasema alijua hukumu ilikuwa muhimu akajipa matumaini kuwa ataachiwa huru kwa kuwa aliamini hakutenda kosa hilo.

“Ni kama kwenye mpira, nilikuwa najitathmini kati ya mashahidi 29 hakuna aliyenizungumzia zaidi ya askari aliyenikamata nikawa najipa matumaini. Na hata askari wenyewe wanavyosema huyu hakuhusika nikawa najipa matumaini ya 50/50 naweza kutoka au nikafungwa lakini kwa ujumla huwezi kuwa sawa hata kidogo,” anasema.

Anasema uzoefu wa kuingia mahakamani wakati wa usikilizaji wa kesi na kuona nyingine zinavyoamuliwa,  aliona mwenendo wa Jaji Kevin Mhina ukamsaidia kujiamini anaweza kuachiwa.

“Mfumo wa jaji unabadilika kuna wakati anaanza na mepesi na mwisho anaingia kwenye ugumu na mengine anaanza na ugumu lakini mwisho mtu anaachiwa huwezi kutabiri sana hukumu linaweza kuanza na mambo mepesi unaweza kufurahi likafika sehemu linabana na ikaishia kwenye kifungo,” anasema.

“Mfano shauri letu, Jaji alianza mteremko akafika mahali ukaona kama gari linaweka breki, alipoanza kupanda nilikaribia kupoteza fahamu kwa sababu alipokaribia mwishoni alisoma mtuhumiwa wa kwanza alivyofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wote. Upande wa Jamhuri wamethibitisha pasipo shaka, aisee! nilikaribia kuanguka mwili hauna nguvu kabisa roho tu ndiyo ilibaki na matumaini,” anasema.

“Hadi aliposema kwa maana hiyo, mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu… ndipo nguvu ikaanza kurudi maana najua unapotaja kitu ukaweka na, unakuwa umekaribia mwisho nilivuta pumzi kwa nguvu matumaini yakarudi.

Anasema ghafla hali ilibadilika alipomsikia Jaji Mhina akisema: “Mahakama inamwachia huru mshtakiwa wa nne, Musa Pastory.”

“Nilishindwa kuamini, hisia zangu zikachanganyika kati ya furaha na mshangao hata nilipokuwa nikijitahidi kujituliza nilishindwa kujizuia kutokwa machozi ya furaha. Sikuamini nilitamani niruke sikuwa sawa kabisa,” anasema.

Je, ni kweli alikuwa na mahusiano na washtakiwa wengine? Pastory anasema hawezi kusema alikuwa na mahusiano na wenzake watatu waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa kuwa ni ukweli kuwa hakuwahi kuonana nao wala kujua historia yao lakini amewahi kuwasiliana na mshtakiwa wa pili, Safari Lubingo.

Anasema, “subira ndiyo neno kuu nimejifunza katika kesi hii. Ukiwa na subira au kuvumilia ni jambo nzuri, tangu nimeingia mwaka jana nimeshuhudia mengi, watu wanakimbia wanakamatwa wengine wanaanguka kwa presha na wakati mwingine wanaingia kwenye matatizo lakini wangevumilia wasingeingia kwenye matatizo.’’

Anasema ni vyema mtu akiwa gerezani atazame kesi iliyo mbele yake badala ya kuwaza yaliyo nje yanaweza kumsababishia matatizo ya kiafya, hata kushawishika kutoroka.

Anasema tangu akamatwe mkewe na ndugu zake walifika magereza kumsalimia kila Jumamosi wanapopewa nafasi lakini aliwaonya wasimpe taarifa zozote za nyumbani au nje ya gereza kwa kuwa hakuzihitaji akisema zingemuumiza.

“Nilimwambia mke wangu asiniambie chochote, huko nje apambane mwenyewe akiweza sawa asipoweza aache ikitokea nimetoka basi nitakutana nalo,” anasema.

Pastory anasema bado ana ndoto ya kuwa mwalimu na amejipanga kuomba kazi, huku akiangalia pia fursa nyingine kwa kuwa anaamini Mungu hampi mtu adhabu mara mbili.

Related Posts