Dodoma. Mashahidi sita wa upande wa Jamhuri wameshatoa ushahidi katika kesi ya ubakaji na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam.
Kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 imeendelea leo Agosti 30, 2024, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa kusikiliza mashahidi watatu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.
Wanaokabiliwa na mashtaka ya kumbaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti huyo anayetambulishwa mahakamani kwa jina la XY.
Washtakiwa walikana mashtaka baada ya kusomewa walipofikishwa mahakamani mara ya kwanza Agosti 19, 2024.
Upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama kusikiliza kesi hiyo mfululizo kwa faragha kuanzia Agosti 20 hadi 23, 2024 kutokana na unyeti wa kesi hiyo.
Agosti 23, kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 28, kupisha shauri la mapitio ya uhalali wa mwenendo wa kesi hiyo ya jinai lililofunguliwa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, na wakili Leonard Mashabara.
Wakili hiyo alikuwa na hoja ya kuwataka washtakiwa wasiwakilishwe na mawakili ambao ni wanachama wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), akidai Baraza la Uongozi la chama hicho liliwataja kuwa wahalifu.
Jaji wa Mahakama Kuu aliyesikiliza shauri hilo, Suleiman Hassan, alilitupa akisema lilikuwa kinyume cha sheria kwa sababu kuna watu ambao hawahusiki kwenye kesi ya msingi lakini walitajwa kuwa miongoni mwa wajibu maombi.
Akizungumza nje ya mahakama leo Ijumaa, Agosti 30, 2024, wakili anayewawakilisha washtakiwa hao, Godfrey Wasonga amesema kesi hiyo itaendelea kuanzia Septemba 2, 2024.
Amesema leo wamesikilizwa mashahidi watatu (hakuwataja majina wala vyeo vyao) ila ni watu waliomsaidia XY alipobakwa na kulawitiwa.
Binti huyo, akiwa shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri, alitoa ushahidi Agosti 22, 2024 mbele ya hakimu Zabibu Mpangule.
Wengine waliotoa ushahidi ni shahidi wa kwanza, mtaalamu wa uchunguzi wa mambo ya sayansi ya simu na vifaa vya kielektroniki kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi na shahidi wa pili, ni daktari kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.