ACHANA na matokeo iliyoanza nayo Ken Gold, straika wa timu hiyo, Joshua Ibrahim amesema bao aliloanza nalo katika Ligi Kuu wakati timu hiyo ikifumuliwa 3-1 na Singida Black Stars limemuongeza nguvu kikosini na kutamba ataendelea kumfunga yeyote kadri msimu utakavyosonga mbele.
Ibrahim aliyewahi kukipiga Tusker ya Kenya alifunga bao hilo katika mechi ya kufungulia msimu kwenye Uwanja wa Sokoine ukiwa ni mchezo wa kwanza wa wageni hao waliopanda daraja kutoka Ligi ya Championship, na sasa wanajiandaa kuifuata Fountain Gate mkoani Manyara, Septemba 11.
Straika huyo aliliambia Mwanaspoti kwamba, licha ya kupoteza mchezo wa ufunguzi wa ligi, lakini haimaanishi wamepoteza michezo yote kwani timu bado ni ngeni kwenye ligi.
Alisema kinachompa hamasa na nguvu ni jinsi alivyoanza ligi kwa kufunga, jambo ambalo linampa matumaini ya kufanya vizuri na kuendelea kufunga.
“Kimsingi hatuwezi kukata tamaa bado ni mapema. Pamoja na kupoteza mechi ya kwanza, lakini tulipata bao jambo linalonipa faraja ya kuendeleza kufunga mabao mechi zijazo. Kazi ya straika ni kuweka mpira wavuni, nashukuru tumekuwa na ushirikiano na wenzangu kuipambania timu kuhakikisha tunamaliza katika nafasi nzuri,” alisema Ibrahim.
Kocha wa timu hiyo, Fikiri Elias alisema kwa kwa sasa anaendelea kuwaandaa wachezaji kisaikolojia, kutengeneza muunganiko na utimamu ili kuhakikisha mechi zinazofuata wafanye kweli.
“Tunaendelea na mazoezi kurekebisha makosa yaliyoonekana na kutengeneza kombinesheni ili mechi zinazofuata tuweze kufanya vizuri. Naamini timu itakuwa imara,” alisema Elias aliyewahi kuinoa Coastal Union.