TPA kuanza kukusanya tozo ya ‘wharfage’

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuanzia Septemba mosi 2024 itaanza kukusanya malipo ya tozo ya matumizi ya miundombinu ya bandari (wharfage) kwa mizigo yote.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na TPA leo Ijumaa Agosti 30, 2024 kupitia kwenye vyombo vya habari, imesema hatua hiyo inatokana na mabadiliko ya sheria.

Kutokana na mabadiliko hayo, TPA imesema: “Shehena inayoingia nchini, baada ya kukamilisha taratibu za kuwasilisha kadhia ya forodha, mteja anapaswa kuingia kwenye akaunti yake katika Mfumo wa Pamoja wa Kielektroniki wa Uondoshaji Shehena Maeneo ya Forodha (TeSWS) au Mfumo wa Malipo wa TPA (TePP) kupata ankara ya tozo ya wharfage kwa ajili ya kufanya malipo.”

Baada ya malipo kufanyika, TPA imeeleza mteja ataendelea na taratibu za kupata kibali cha kutoa mzigo kutoka TRA na hivyo kutoa mzigo bandarini baada ya kukamilisha malipo ya mwendeshaji bandari.

“Ifahamike kwamba kwa mizigo yote iendayo nje ya nchi, malipo kwa ajili ya tozo ya wharfage yatalipwa kwa dola (za Marekani),” imeeleza TPA.

Mamlaka hiyo imesema ni muhimu kuzingatia kuwa mteja hataweza kupata kibali cha kutoa mzigo bila kukamilisha malipo ya tozo hiyo.

Kuhusu shehena inayokwenda nje ya nchi, TPA imesema baada ya kumaliza taratibu zote za kuwasilisha kadhia za kiforodha za upakiaji mzigo na kabla ya kuingiza mzigo bandarini, mteja anapaswa kuingia kwenye akaunti yake katika mfumo wa TeSWS au TePP ili kupata ankara ya TPA kwa malipo ya wharfage.

“Taratibu za kiforodha za kuingiza shehena bandarini zitaweza kufanyika pale tu malipo ya tozo ya wharfage yatakuwa yamekamilika,” imeeleza taarifa hiyo.

Kutokana na mabadiliko hayo, TPA imetoa wito kwa wadau na wateja wake wanaohusika na uondoshaji wa shehena bandarini kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji ili kuwezesha bandari kuendelea kutoa huduma bora kwa masilahi ya pande zote na Taifa kwa ujumla.

Menejimenti ya TPA imewahakikishia wateja, wadau na umma kuwa itaendelea kutimiza wajibu wake wa kutoa huduma bora wakati wote, na kushirikisha wadau kuwezesha shughuli za kibandari kufanyika kwa tija na ufanisi.

Related Posts