LICHA ya kukiri ugumu uliopo katika ligi ya Championship, kiungo wa Mtibwa Sugar, Abdul Hilary amechimba mkwara kwa kusema hakuna timu ambayo inaweza kuwafanya kuwa na presha juu ya mpango wao wa kurejea Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026.
Mtibwa iliyowahi kutwaa ubingwa wa Bara misimu miwili mfululizo ya 1999 na 2000 ilishuka daraja msimu uliopita sambamba na Geita Gold na msimu huu itashiriki Ligi ya Championship, inayotajwa kuwa ngumu, lakini nyota huyo wa zamani wa KMC na Tusker ya Kenya, alisema kilichotokea msimu uliopita kimepita kwa sasa fikra na mawazo yao zipo katika namna ya kurejea tena Ligi Kuu.
“Niseme ukweli tumekuwa na maandalizi mazuri mabayo yananifanya kuwa na imani kubwa kwamba kurejea ligi kuu ni suala la muda tu kwetu,uzuri kikosi chetu kipo pamoja bado ni wachezaji wachache waliondoka,” alisema Hilary na kuongeza;
“Najua ugumu uliopo katika ngazi hii ya soka (Championship) lakini kwetu sio tatizo na wala hakuna timu ambayo ninahofu nayo kwakweli kama tumekuwa na uwezo wa kucheza vizuri dhidi ya timu za ligi kuu na kupata matokeo mazuri ni imani yangu hata huku napo tutaweza na kufanikisha mpango wetu.”
Katika kipindi hiki cha maandalizi na msimu ujao wa Championship ambao unatarajiwa kuanza mwezi ujao, Mtibwa inayonolewa na kocha Melis Medo imecheza michezo kadhaa ya kirafiki ikiwemo dhidi Singida Black Stars ambayo inashiriki Ligi Kuu Bara na kuinyuka mabao 2-0.
Akiongelea maandalizi ya timu hiyo, Medo alisema yanaenda vizuri na michezo ya kirafiki wanayoendelea kucheza inaendelea kukiimarisha zaidi kikosi hicho kiushindani; “Tupo tayari hata kesho kuanza msimu mpya, ninafuraha na namna ambavyo vijana wanapambana na kuonyesha uwezo wao.”
Mtibwa ilianzishwa mwaka 1988 na kundi la wafanyakazi wa Mtibwa Sugar Estates Ltd na ilishiriki mashindano ya ligi ngazi ya wilaya na ilipanda Ligi Daraja la Kwanza sasa Ligi Kuu mwaka 1996 na kubeba ubingwa 1999 na 2000 ikiwa ndio timu pekee kutetea taji nje ya vigogo Simba na Yanga.