Dar es Salaam. Baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii ya X, Facebook na Instagram wamesimulia namna wanavyopitia kadhia ya majaribio ya kutapeliwa na watu wasiojulikana.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti wamesema kupitia mitandao hiyo kuna wimbi la watu wanaowashawishi kuingia katika biashara mtandao ya pesa zijulikanazo kama Cryptocurrency pamoja na utapeli mwingine.
Jamal Ramadhan amesema aliwahi kushawishiwa kujiunga na biashara ya sarafu mtandao ya Forex na mtumiaji wa mtandao wa X, baada ya mtumiaji huyo aliyeweka picha ya dada wa Kichina kumtumia ujumbe kwenye ukurasa wake.
Anasema mtumiaji huyo alimwambia ajiunge na Forex ambapo atapata faida ya fedha maradufu huku akimtaka ampatie barua pepe na maelezo mengine binafsi.
Anasema biashara hiyo ingemuhitaji anunue na kuuza pesa za mtandaoni.
“Kuna dada wa Kiarabu aliingia kwenye ukurasa wangu wa mtandao wa Instagram alianza kunifuatilia na ku-like picha zangu, akanitumia sms tukaanza kuwasiliana kumbe alikuwa na lengo la kunitapeli,” amesema Dennis Emmanuel.
Emmanuel amesema ilikuwa mwaka 2020 na walitumia miezi sita kuwasiliana hadi kwenye mtandao wa WhatsApp hadi alipokuja kugundua kuwa ni tapeli. Amesema alikuwa akimuomba fedha mara kwa mara.
Baraka Teleza, kwa upande wake amesema Agosti 28, 2024 alifuatwa na mtumiaji wa Mtandao wa Facebook akimtaka namba yake ya mtandao wa Whatsapp.
“Nilipompatia namba yangu akanitumia picha zake za mitego huku akijionyesha ni mtu mwenye pesa na mali ambapo dhumuni lake akimtaka awekeze kwenye biashara ya sarafu za mtandao.
Aidha, anasema ametumia utaalamu wa kujua mwenye picha hizo kupitia Google Scan ambapo amegundua kuwa si muhusika halisi wa picha hizo.
Mwingine ni Belinda Michael anayesema alitafutwa kwenye mtandao wa Facebook na mtu anayeitwa Elizabeth aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa nchini Ujerumani akitaka namba yake ya WhatsApp:
“Baada ya kumtumia namba yangu aliniomba nimtumie namba za mtandao wa Telegram nilizotumiwa kama Nywila ili aweze kuingia kwenye ukurasa wangu wa Telegram kwa ajili ya kazi zake za ulaghai lakini nikamkatalia,” amesema.
Kutokana na hilo, ofisa mwandamizi mkuu wa mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala alipouliwa na Mwananchi amesema:
“Mitandao ya kijamii imerahisisha huduma nyingi za kijamii na imeongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma mbalimbali na kasi ya maendeleo kwa wananchi, jamii na Taifa kwa ujumla, lakini mbali na hayo, kuna utapeli na wizi unaoendelea katika mitandao hiyo.
“TCRA kama mamlaka ya mawasilliano inatoa tahadhari kupitia njia mbalimbali, ikiwemo kampeni inayoendelea iitwayo, ‘Mitandao ni fursa baki salama’, ukiwa na lengo la kuonyesha fursa mbalimbali zinazopatikana katika mitandao ya kijamii, lakini pia kukumbusha umma kujilinda juu ya wizi na utapeli wa mitandao hii,” amesema.
Amesema pia TCRA inatoa tahadhari kuwa, “Usitoe pesa wala kufanya biashara na mtu yeyote uliyekutana naye katika mitandao ya kijamii, bila kujali cheo au ahadi alizokutajia mtu huyo. Jukumu la ulinzi na usalama wa mali zetu ni letu sote.”
Awali, mwaka 2022, TCRA ilizindua kampeni ya elimu kwa umma ikiwa na lengo la kuwakumbusha na kuwaelimisha watumiaji wa huduma za mawasiliano na wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia huduma hiyo kwa umakini ili kuepuka wizi na ulaghai wa kimtandao.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Jabiri Bakari anasisitiza dhamira ya taasisi anayoisimamia na kuiongoza kuwa inahakikisha mazingira ya kimtandao yanakuwa salama, ili yawe yenye kuchangia ukuaji wa uchumi wa kisasa na wakidijitali.