Zahera, Namungo lolote linaweza kutokea

NAMUNGO imepoteza mechi ya pili mfululizo katika Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kufungwa mabao 2-0 na Fountain Gate na ghafla Mtendaji Mkuu, Omar Kaya akatangaza kuachia ngazi na uongozi wa juu kuridhia.

Lakini, kwa sasa lolote linaweza kutokea kwa kocha mkuu, Mwinyi Zahera.

Namungo ilikumbana na kipigo hicho juzi usiku kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi ukiwa ni mchezo wa pili mfululizo ikilala nyumbani baada ya awali kufumuliwa 2-1 na Tabora United, matokeo yaliyoushtua uongozi na kuamua kumuweka kiti moto Zahera, saa chache baada ya Kaya kujiuzulu.

Kaya kupitia ukurasa wake wa Instagram alitangaza uamuzi huo kwa kuandika ‘Mimi Omar Kaya siku ya leo tarehe 30 Aug 2024 nimewasilisha kwa uongozi barua ya kujiuzulu nafasi ya utendaji mkuu wa Klabu ya NamungoFC…

‘Hivyo napenda kuwashukuru uongozi, benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wote wa Klabu ya Namungo katika kipindi chote nilichoitumikia kwa ushirikiano wao kama familia.

‘Niwatakie safari njema katika kutimiza malengo ya Klabu Inshaallah…’

Na muda mfupi baada ya taarifa yake uongozi wa klabu hiyo ulitoa ya kuridhia kuachia ngazi kwa katibu mkuu huyo wa zamani wa Yanga na taarifa zaidi zinasema kwa sasa ni suala la muda kwa kocha Mwinyi Zahera kutimuliwa.

Chanzo cha ndani ya timu hiyo kimesema ilikuwa atangulie Zahera kabla ya Kaya, na inaelezwa sababu kuu ni kwamba kocha huyo alipewa jukumu la kusajili wachezaji aliowaona watamfaa ili kuhakikisha timu inapata matokeo ya ushindi, hivyo kufungwa mechi mbili mfululizo wanaiona ni ishara  itakayokwamisha malengo ya msimu huu.

“Kila kitu alichiwa akifanye, lakini tunaona haijawa vile tulivyotarajia. Ameambiwa aandike barua ya kuachia ngazi, hilo alipaswa alifanye kabla ya uamuzi wa Kaya aliyeamua kuwajibika,” kilisema chanzo hicho.

“Ni bora kuondoa changamoto mapema kuliko kusubiri ikuumize mbele ya safari. Malengo ya Namungo msimu huu ni kupigania nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.”

Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Ally Selemani alipotafutwa na Mwanaspoti kujua kipindi hiki nani atakaimu nafasi ya Kaya, alisema leo watakutana ili kufanya uteuzi, lakini kwa ishu ya Zahera itakapokamilika watautangazia umma.

“Kama Zahera anaondoka au la mtajulishwa mara litakapokamilika, lakini kwa mtu wa kukaimu au kurithi nafasi ya CEO tunatarajiwa kukutana kesho (leo) kufanya uamuzi,” alisema.

Alipotafutwa jana na gazeti hili, simu yake iliita bila kupokewa na alipotumiwa ujumbe hakuujibu licha ya kuonekana ameupokea na kuusoma.

Related Posts