Afungwa maisha jela kwa kumlawiti mtoto wa miaka miwili

Mbulu. Mkazi wa kijiji cha Moringe, mkoani Manyara, Carol Christopher (18) amehukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya Wilaya ya Mbulu kwa kumlawiti mtoto wa miaka miwili na miezi nane.

Hata hivyo, Carol hakuwepo mahakamani wakati wa hukumu hiyo iliyotolewa Agosti 30 na kusababisha mama yake ambaye ni mdhamini wake kuhukumiwa miezi sita gerezani.

Mama huyo Anna Burra aliyekuwa amemdhamini anatumikia kifungo cha miezi sita jela baada ya kushindwa kulipa Sh3 milioni ya dhamana aliyokuwa amemuwekea Carol.

Mama huyo amebainika kuwa aliidanganya mahakama kuwa mshtakiwa amelazwa katika hospitali ya Seliani mkoani Arusha na kushindwa kutoa vielelezo mahakamani ili kuthibitisha ugonjwa.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na mkaguzi wa Polisi, Maraba Masheku uliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe funzo kwa jamii,  akitilia msisitizo kuwa Serikali inatumia nguvu kubwa kukemea na kutoa elimu kwa kuzingatia kifungu cha sheria 154 (2) Sura ya 16, lakini pia mshtakiwa ni mtu mzima aliyemfanyia ukatili mtoto chini ya umri wa miaka 10.

Akitoa hukumu huku Mahakama hiyo ikitoa hati ya kumtafuta mshtakiwa ili afikishwe mahakamani kusomewa shtaka lake, hakimu Johari Kijuwile amesema hukumu hiyo imezingatia upande wa utetezi wa mashahidi wanne kushindwa kuithibitisha mahakama hiyo, ila upande wa mashtaka uliowasilishwa na mashahidi sita ukithibitishia ukatili aliotendewa mtoto huyo.

Hakimu Kijuwile amesema japo shahidi namba tano ambaye ni mtoto hakuweza kuzungumza ila mahakama imetumia busara ya kuzingatia maoni, hivyo imelazimika kutoa hukumu ya kifungo cha maisha gerezani.

Related Posts