Hayo yameelezwa na mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus baada ya kurejea siku ya Ijumaa kutoka nchini Kongo huku akisema kuwa katika siku zijazo chanjo zaidi zitawasilishwa nchini humo.
Agosti 14 mwaka huu, WHO ilitangaza hali ya dharura ya kimataifa kutokana na kusambaa kwa virusi vya mpox, hasa kuongezeka kwa visa vya maambukizi vya aina mpya ya virusi hivyo inayofahamika kama Clade 1b nchini Kongo na katika nchi jirani.
Soma pia: Papa Francis atoa mwito wa msaada zaidi kwa wagonjwa wa mpox
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani – WHO, karibu visa 15,000 vya mpox vimegundulika nchini Kongo katika mwaka wa 2024, huku kukiwa na vifo 500.
Mataifa mbalimbali yaahidi kuisaidia DRC kupambana na Mpox
Serikali ya Ujerumani imesema itapeleka Kongo maabara ya kuhamishika ili kusaidia kuwagundua wagonjwa wa homa ya Mpox na kudhibiti kuenea kwa maambukizi.
Soma pia: Ufadhili wa mapambano ya Mpox Afrika wachechemea
Wizara ya Ushirikiano wa Kimaendeleo wa nchi hiyo imesema pia kuna mipango ya kutoa mafunzo kwa wataalamu zaidi ili waweze kutambua dalili na kuufahamisha umma kuhusu hatua za kuzuia ugonjwa huo.
Kwa upande mwingine, Serikali ya Uingereza iliiahidi siku ya Jumatano Kongo kitita cha pauni milioni 3.1 kwa ajili ya kusaidia kupambana na mripuko wa homa ya Mpox ambao tayari umeshauwa watu zaidi ya 500 na kuathiri wengine kadhaa.
(Vyanzo: AP, DPAE, AFP)