NA WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni amelazimika kufunga Jengo lililokuwa likitumika kama nyumba ya ibada maarufu “KANISA LA NABII ELIA MSANGI” baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa kanisa hilo linaloendeshwa kinyume na taratibu za sheria ya Nchi lakini pia kudaiwa kuwepo vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, na vitendo vingine vya Mmomonyoko wa maadili.
Ametoa maagizo hayo wakati wa ziara yake alipoambatana na kamati ya Usalama ya Wilaya walipotembelea eneo lilipo kanisa hilo kitongoji cha Ikongwe A kata ya Msindo kujiridhisha na taarifa za kuwepo viashiria vya matukio yasiyofaa yanayodaiwa kufanyika kwenye nyumba hiyo inayotumika kama kanisa na kubaini hakuna usajili wowote.
Akizungumzia kufungwa kwa kanisa hilo Mkuu huyo wa wilaya amesema miongoni mwa sababu za kufunga kanisa hilo ni kuendeshwa pasipokuwa na usajili hali ambayo imepelekea kutojulikana kama ni dhehebu gani la kidini, lakini pia hata uongozi unaosimamia kanisa hilo haujulikani mahali popote kwakua halipo kwenye orodha ya taasisi za kidini zilizosajiriwa.
“Jumuiya au Taasisi yoyote ya Kidini ili iweze kufanya kazi lazima isajiliwe kwa hiyo hili kanisa lenu halijasajiliwa kwa mantiki hiyo linaendeshwa kinyume cha sheria kwa sababu hakuna taarifa zozote za ziada ikiwemo usajili na namna linavyo endeshwa hivyo kuanzia leo hakuna kuendesha ibada wala shughuli yoyote kwenye jengo hili”. Alisema mkuu wa Wilaya ya Same.
Kwa mujibu wa maelezo ya baadhi ya wazee akiwemo Mzee Agustino Karaba Karugwe ambae alishuhudia maisha ya Nabii Elia Msangi Mwanzilishi wa Kanisa hilo ambae alifariki April 9 mwaka 1996, mpaka kifo chake alikuwa amezaa na wanawake 14 na ana watoto zaidi ya 70 baadhi yao wanaendelea kuishi hapo na wengine waliamua kuondoka kwenda kutafuta maisha maeneo mengine baada ya kutoridhishwa na vitendo vinavyoendelea kwenye eneo hilo.
Imefahamika kuwa katika kanisa hilo haruhusiwi mtu yeyote kutoka nje ya kitongoji hicho kwenda kusali katika kanisa hilo isipokuwa wanajumuia walioko ndani ya kitongoji hicho , na haruhusiwi kuingia yeyote isipokuwa kwa ruhusa na kuna geti maalum la kuingilia katika kitongoji hicho na wakati wote huwa limefugwa.