KAMA ulikuwa unajiuliza maswali kuhusu kutokuonekana uwanjani kwa mshambuliaji mpya wa Simba Leonel Ateba basi majibu yamepatikana,baada ya kocha wake Fadlu Davids kusisitiza kuwa alikuwa jikoni sasa ameiva.
Mcameroon (25) huyo mwenye uwezo wa kucheza kama winga wa kushoto na kulia na mwenye sifa ya kuwa mchezaji wa kipekee mwenye uwezo wa kushambulia kutoka pande zote za uwanja ndiye mchezaji wa mwisho kusajiliwa Simba akitokea USM Alger.
Ameondoka katika kikosi hicho akiwa na rekodi ya kucheza mechi 23 katika michuano mbalimbali na kufunga mabao matatu na kutoa asisti saba akiwa kwenye nafasi hiyo hiyo ya ushambuliaji.
Akizungumza na Mwanaspoti kocha Fadlu alisema, Ateba alikuwa nje kwa sababu ya vibali vyake havikuwa tayari lakini pia hakumpa mechi za hivi karibuni kwani alikuwa bado hajawa na utimamu.
Alitaka kumuweka sawa na kumfanya aelewane na wenzake, aielewe timu kwani alifika wakati wachezaji wenzake wote wameshakaa pamoja kwa muda mrefu na kufanya mazoezi ya kutosha.
“Nilitaka apate mazoezi ya kutosha ya kumuweka sawa kabla kuanza kucheza katika mechi yoyote ile, kwa sasa anaendelea kuimarika ninataka kumpa nafasi kwenye mchezo dhidi ya Al Hilal ili aanze kuingia kwenye mifumo ya timu.
“Naamini Ateba ataongeza kitu kizito kwenye safu ya ushambuliaji pia mchezo wa Al Hilal ni muhimu kujiandaa, ikiwa ni mchezo wa kwanza kwenye hatua hii ya michuano ya kimataifa hivyo tunahitaji ushindi na wachezaji wenye hari na morali isiyo ya kawaida,” alisema Fadlu.
Ujio wa Ateba ulimuondoa Freddy Koublan ambaye msimu uliopita alitua Simba dirisha dogo na kufunga mabao sita ya ligi, huku hiyo ikimpa kazi ya ziada ya kuvuka rekodi za mwenzake aliyepita.
Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana, ila asili yake ni Uganda alisajiliwa hivi karibuni akiwa na rekodi ya kufunga mabao 14 na asisti mbili msimu uliopita, huku akiwa na sifa ya kufunga mabao ya aina zote na katika mechi mbili ilizocheza Simba amefunga bao moja.
Valentino Mashaka (20) kutoka Geita Gold .Msimu uliopita alifunga goli 6,Assit 1,mechi 24 sawa na dk 1499 na katika mechi mbili ilizocheza Simba amefunga bao moja..
Mrithi wa Freddy, Lionel Ateba kutoka USM Alger, ambaye hakuwa anapata nafasi ya kucheza katika kikosi hicho kabla ya kutimkia Simba msimu huu, aliichezea Dynamo Douala FC ya kwao Cameroon, huku akitoka na rekodi ya kuhusika katika jumla ya mabao tisa, akifunga moja na kuasisti manane katika michezo 16.
Simba imekuwa na mfululizo wa kuondoa washambuliaji walio na rekodi nzuri, msimu uliopita ilimuondoa Saido Ntibazonkiza, Jean Baleke dirisha dogo wote wakiwa na mabao saba.