MWENYEKITI wa Pamba Jiji, Bhiku Kotecha amesema bado wana imani kubwa na benchi la ufundi na wachezaji na hawawezi kukurupuka kufanya mabadiliko ya haraka kwa kuzingatia matokeo ya mechi mbili za Ligi Kuu, huku akiahidi mambo mazuri.
Pamba inakamata nafasi ya sita katika Ligi Kuu ikiwa na alama mbili baada ya kutoka suluhu dhidi ya Dodoma Jiji na Tanzania Prisons, ilhali ikiwa haijafunga wala kuruhusu bao licha ya nyota wa timu hiyo, kipa Yona Amos na straika George Mpole kuibuka nyota wa michezo hiyo.
Kotecha alisema wiki mbili za mapumziko kupisha mechi za timu za taifa, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, timu hiyo itacheza mechi tatu za kirafiki kujiweka fiti dhidi ya Geita Gold, Stand United na Biashara United.
“Tunaarajia kucheza na Geita Gold, Stand United na mambo yakienda vizuri tutacheza pia na Biashara United, kwa sasa mazoezi yanaendelea kila siku katika uwanja wa Nyamagana kwahiyo tunajipanga vizuri wala hakuna shida yoyote,” alisema Kotecha
Aliongeza kwa sasa ni mapema kukosa imani na kikosi chao katika mechi mbili walizocheza kwani kuna maendeleo yanaonekana na timu inabadilika kila mchezo, huku akiwataka mashabiki kuwa wavumilivu na kuiunga mkono timu yao.
“Ni timu ambayo ni mara ya kwanza inashiriki siku zinavyoenda inabadilika mimi naamini itafanya vizuri isipokuwa watu waiamini, waamini benchi la ufundi kwa sababu huwezi ukaingia tu siku moja ukafanya vizuri mpira una matokeo matatu,” alisema Kotecha.
“Hatujapoteza mchezo na hatujaruhusu bao hiyo nayo ni sifa hata kwenye msimamo hatuko mbali na aliye juu. Sisi tumejipanga kushinda na tuko wananchi wawe na imani na Pamba na benchi la ufundi mambo yatakwenda vizuri.”