MAMA KOKA KUTUA KERO NA CHANGAMOTO ZINAZOIKUMBA SHULE YA MSINGI MKUZA

NA VICTOR MASANGU,KIBAHA 

Mke wa Mbunge la Jimbo la Kibaha mjini Mama Selina Koka katika kuboresha sekta ya elimu ameahidi kuzivalia njuga   baadhi ya changamoto mbali mbali zinazoikabili shule ya msingi Mkuza.

Mama Koka ametoa ahadi hiyo wakati wa sherehe za mahafali ya  kuhitumu wanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Mkuza iliyopo katika Halmashauri ya mji Kibaha.

Alisema kwamba dhamira yake kubwa ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kupambana na kuboresha sekta ya elimu.

“Mimi kama mke wa Mbunge nitajitahidi kwa hali na mali pamoja na familia yangu kusaidia mahitaji mbali mbali kwa upande wa wanafunzi pamoja na walimu wa shule hii ya mkuza,”alisema Mama Koka.

Aliongeza kwamba anatambua shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali na kuongeza kuwa ataanza kusaidia mahitaji mbali mbali ya msingi ikiwemo mtambo maalumu wa kutolea nakala ‘Photocopy mashine’ ambayo itawasaidia katika kuendeshea kazi zao mbali mbali.

Kadhalika alimpongeza Rais  Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutenga fedha nyingi ambazo zimeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo katika Jimbo la Kibaha mjini.

Katika hatua nyingine Mama Koka alitoa zawadi mbali mbali kwa wanafunzi wa shule hiyo ambao wameweza kufanya vizuri katika masomo yao ikiwa pamoja na kuwapatia zawadi ya vitenge wazazi pamoja na walimu kwa kufanya kazi nzuri ya kuwatunza na kuwalea watoto.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo ya msingi Mkuza amempongeza kwa dhati Mama Selina Koka kwa jitihada zake za kushirikiana na walimu katika kuboresha sekta ya elimu.

Aidha Mwalimu huyo pamoja na hayo hakusita kueleza baadhi ya changamoto zinazowakabili zikiwemo uhaba wa vyumba vya madarasa,uhaba wa matundu ya vyoo,pamoja na uhitaji wa tenki la kuhifadhia maji.

Alimuomba pia asaidiwe kutatuliwa changamoto hizo ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo ya madarasa ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira rafiki.




Related Posts