WACHEZAJI wa JKT Tanzania baada ya kupata suluhu mechi ya kwanza dhidi ya Azam FC iliyopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, wamejua kipi wakifanye ili waanze kuvuna pointi tatu michezo ijayo.
Nahodha wa timu hiyo, Edward Songo alisema haikuwa kazi rahisi katika mechi hiyo, kwani kila timu ilipania kuanza na ushindi, hivyo michezo iliyopo mbele anaamini itawapa kicheko mashabiki wao akitamba kuwa kazi imeanza waendelee kuwaunga mkono.
“Kila mchezaji alikuwa na hamu ya kuhakikisha tunashinda dhidi ya Azam FC isitoshe tulicheza nyumbani, lakini matokeo ya suluhu yametupa picha kipi tutakifanya katika mechi zinazofuata,” alisema.
Mchezaji mwenzake, Maka Edward anayecheza nafasi ya kiungo alisema wamepata picha kamili ya jinsi ligi ya msimu huu ilivyo ngumu, hivyo wanajipanga kuhakikisha michezo iliyo mbele inakuwa ya kuvuna pointi tatu.
“Mahesabu yanatakiwa kuanza mapema iwezekanavyo ili kujiweka katika mazingira ya malengo ya timu kwa msimu huu, hivyo kila mechi kwetu ni funzo la kuboresha viwango,” alisema Maka.
JKT iliyoponea kushuka daraja msimu uliopita kupitia mchujo (play-off) kwa kuifunga Tabora United iliyoenda kujitetea mbele ya Biashara United, huu ni msimu wa pili tangu iliporejea katika ligi hiyo ikitokea Ligi ya Championship sambamba na Mashujaa na Tabora United iliyokuwa ikifahamika kama Kitayosce.
Maafaande hao watasafiri hadi mjini Bukoba, Septemba 16 ili kuvaana na Kagera Sugar iliyoanza msimu kwa vipigo viwili mfululizo ikiwa nyumbani mbele ya Singida Black Stars na Yanga.