Dar es Salaam. Wadau wa biashara wameeleza kuwa kampuni changa nchini zinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mtaji, jambo ambalo linaathiri uendelevu wake.
Wanasema ili kupata mitaji wanategemea kukopa lakini mfumo wa benki nchini bado unahitaji dhamana kubwa kabla ya kutoa mikopo, hali inayowafanya kushindwa kupata fedha zinazohitajika kuendesha biashara zao.
Akizungumza juzi katika mkutano wa kuendesha uwekezaji wa Tanzania kupitia hisa binafsi, Mkurugenzi Mtendaji wa Africapital Investment Holding Ltd, Burak Buyuksarac amesema kuna haja ya wafanyabiashara wachanga, kujikita kwenye mitaji ya ubia kwani dhamana za mali zisizohamishika ambazo ni pamoja na ardhi, majengo na mali nyingine ni vigumu kupatikana.
“Katika mazingira haya, mitaji ya ubia imejitokeza kama suluhisho muhimu. Tofauti na benki, kampuni za mitaji ya ubia haziangalii dhamana bali zinajikita zaidi katika uwezo wa kampuni kukua na kutoa faida kwa muda mrefu,” amesema Buyuksarac.
Naye, Mkurugenzi wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike amesema katika mazingira ya sasa ya kibiashara mitaji ya ubia maarufu ‘Ventre Capital’ imekuwa nguzo muhimu kwa kampuni nyingi zinazoanza ambazo zina uwezo wa kukua kwa kasi.
“Mitaji ya ubia imechukua nafasi muhimu ya kuwa wawekezaji wa awali wanaobeba dhamana ya kuwawezesha wajasiriamali kuendeleza biashara zao na kuzifikisha kwenye viwango vya juu zaidi,” amesema Mtambalike.
Amesema kwa ujumla, mitaji ya ubia imekuwa chombo muhimu katika kusaidia kampuni nyingi zinazoanza kukua na kufikia viwango vya juu katika soko la hisa.
Kadhalika, wanaoingia kwenye mitaji ya ubia wanasaidia kuunda kizazi kipya cha kampuni zinazoweza kukua na kutoa ajira nyingi kwa jamii, hivyo katika ulimwengu wa biashara wa sasa, nafasi ya yao ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote
Mkurugenzi Mtendaji wa Raman, Iain Usiri amesema safari ya kupata mtaji wa ubia kwa kampuni kama Ramani haikuwa rahisi. Mwanzoni, mojawapo ya changamoto kubwa ilikuwa kuwashawishi wawekezaji wa kimataifa kuhusu uhalali wa kufanya biashara nchini Tanzania.
“Swali la kwanza nililoulizwa na wawekezaji ni kwa nini tunafanya kazi Tanzania na sio nchi nyingine kama Kenya au Nigeria,” amesema Usiri.
Amesema ilikuwa kazi kubwa kuwaeleza wawekezaji kuhusu fursa zilizopo katika soko la Tanzania, na kuwafanya waone thamani ya kuwekeza katika nchi hii.
Ili kupata mtaji amesema waliamua kuanzisha kampuni mama nchini Marekani na kuifanya kampuni ya Tanzania kuwa tanzu yake. Hii ilisaidia katika kuvutia uwekezaji kutoka kwa wawekezaji wa kimataifa, ambao walijisikia salama zaidi kuwekeza kupitia mfumo wa kisheria wa Marekani.
Mkurugenzi wa utafiti, sera, na mipango, Alfred Mkombo amesema Serikali imeweka mikakati ya kuimarisha sekta ya mitaji ya ujasiriamali na umiliki binafsi kwa kuanzisha mfumo wa kisheria na mipango ya maendeleo.
“Moja ya hatua muhimu ni kuanzisha hifadhi ya mitaji ya ujasiriamali kitaifa na kuunda mazingira yanayowezesha ukuaji wa sekta hii,” amesema Mkombo.
Pia, amesema Serikali inajitahidi kuboresha mfumo wa kisheria na kuboresha mazingira ya biashara ili kuvutia mtaji wa kimataifa.