KOCHA Mkuu wa Fountain Gate FC, Mohamed Muya amesema baada ya kuonja ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu, anatengeneza muunganiko mzuri katika safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Edgar William na Seleman Mwalimu ‘Gomez’.
Nyota hao waliipatia timu hiyo ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo Agosti 29, kwenye Uwanja wa Majaliwa huku kila mmoja akifunga bao moja, jambo lililomfurahisha Muya kutokana na kiwango walichoonyesha.
“Ni wachezaji wazuri na wadogo ambao wana malengo makubwa sana katika taaluma yao ya soka. Nimefurahishwa na aina nzuri ya uchezaji wao, hivyo naamini kadri wanavyozidi kucheza pamoja watatengeneza pacha bora msimu huu kwenye ushambuliaji,” alisema.
Muya aliongeza kuwa katika kipindi cha mapumziko kupisha michezo ya kimataifa, hawatakuwa na mapumziko sana isipokuwa itakuwa ni kwa siku tatu hadi nne tangu mara ya mwisho walipocheza ili kuendelea na mazoezi ya kujiweka fiti zaidi.
“Baada ya michezo miwili ya ugenini dhidi ya Simba na Namungo FC kwa sasa tunajipanga kurejea nyumbani kwenye uwanja wetu wa Tanzanite Kwaraa Manyara, ili kupambana na KenGold Septemba 11, hivyo ni lazima tujipange vizuri kiushindani.”
Edgar alijiunga na timu hiyo msimu huu akitokea KenGold ya Mbeya baada ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita ambapo alikuwa mfungaji bora kufuatia kufunga jumla ya mabao 21, huku akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi ya Championship.
Kwa upande wa Selemani amejiunga na timu hiyo msimu huu baada ya kuachana na KVZ ya Zanzibar na msimu uliopita alikuwa mfungaji bora, kufuatia kufunga mabao 20 na kuchangia (asisti) saba katika michezo 27 kati ya 30 aliyocheza kwenye mashindano hayo.