Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwasilisha miradi minne kwa Serikali ya China kwa lengo la kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada ya utekelezaji wake.
Anatarajia kuiwasilisha katika mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), ambalo kwa miongo zaidi ya miwili sasa limekuwa likitumiwa na wakuu wa nchi za Afrika kwa madhumuni yanayofanana na hayo.
Miradi minne itakayowasilishwa na Rais Samia kwenye mkutano huo ni ujenzi wa mtandao wa mawasiliano vijijini awamu ya pili, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 awamu ya pili na ya tatu, ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi (Veta) awamu ya pili na ujenzi wa barabara za Zanzibar zenye urefu wa kilomita 277.
Taarifa hiyo imetolewa leo Agosti 31, 2024 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam kuhusu ziara ya Rais Samia China.
“Tanzania inatarajia kuwasilisha miradi mbalimbali ikiwemo mipya na ile ambayo haikuweza kutelezwa kwenye mpango uliopita wa FOCAC kwa sababu mbalimbali, ili iweze kupatiwa fedha za mkopo nafuu na msaada na kutekelezwa chini ya mpango kazi wa FOCAC mwaka 2025-2027,” amesema.
Balozi Kombo ametaja malengo matatu ya Tanzania kushiriki mkutano huo; mosi ni kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China ambao mwaka huu umetimiza miaka 60.
Jambo la pili ni kujadiliana na kukubaliana na Serikali ya China namna ya kuendelea kuongeza ushirikiano katika maeneo ya kipaumbele kama sekta ya miundombinu, mifumo ya chakula, biashara na uwekezaji, kubadilishana ujuzi, upatikanaji wa nishati safi na salama na kusaidia ujenzi wa uchumi wa kidijitali.
“Pia kuibua fursa mpya za ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili, kutangaza maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika sheria za sekta ya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi,” amesema.
Akiwa China, Rais Samia atafanya mkutano na Rais Xi Jinping kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
“Aidha, baada ya mazungumzo hayo watashiriki hafla ya kutia saini hati za makubaliano kuhusu kuifufua Reli ya Tazara,” amesema.
Balozi Kombo amesema Rais Samia atafanya mazungumzo na kampuni za China ambazo zipo tayari kufanya uwekezaji mkubwa na kufungua ofisi zao nchini Tanzania.
“Atakutana na kampuni kubwa za China kwa pamoja katika hafla ya chakula cha jioni, yenye lengo la kuhamasisha kufanya uwekezaji nchini Tanzania,” amesema.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo uwekezaji wa China nchini umefikia Sh30 trilioni.
Aidha Tangu kuanza kwake mwaka 2000 FOCAC imewezesha miradi mikubwa ya miundombinu barani Afrika, kama vile ujenzi wa barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari pamoja na uwekezaji katika nishati.
Ushirikiano chini ya FOCAC umeongeza biashara kati ya Afrika na China huku nchi za Afrika zikipata soko kubwa kwa bidhaa zao za kilimo, madini na malighafi nyingine, na kunufaika na uagizaji wa bidhaa za bei nafuu kutoka China.