Takukuru yaibuka na mpya chaguzi zilizopita

Mwanza. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini kwa kuchambua mfumo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020, umebaini kuwepo vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo.

Kauli hiyo imetolewa jana Agosti 30, 2024, Mkuu wa Dawati la Uzuiaji Rushwa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, Stella Bukuru wakati wa mafunzo ya kuzuia rushwa kwa viongozi wa dini mkoani humo.

Ametaja aina za rushwa zilizotawala katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020 kuwa ni pamoja na wagombea kugawa fedha taslimu, vyakula, mbolea na mavazi kama zawadi kwa wapigakura wake, kinyume cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA) Sura ya 329, marejeo ya mwaka 2022.

Kwa mujibu wa Bukuru, utafiti huo ulibainisha kuwa kugawa fedha taslimu kulifanikisha vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo kwa asilimia 64.4, kugawa vitu na vifaa mbalimbali (asilimia 20), kugawa chakula na vinywaji ikiwemo pombe (asilimia 13) na kugawa mbolea (asilimia 2.2).

Bukuru amesema vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi vinapotokea huathiri moja kwa moja uamuzi wa mpigakura kumchagua kiongozi anayeweza kuleta maendeleo kwa jamii na kufanya kazi kwa niaba ya wapigakura wake.

“Vihatarishi vya rushwa vilionekana kwenye maeneo yafuatayo; utangazaji wa majina, wakati wa kujiandikisha na kuandaa orodha ya wapigakura na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali na kwenye utangazaji wa matokeo, mianya iliyochangia vitendo vya rushwa,” amesema Bukuru.

Amebainisha kuwa kutokana na ukubwa wa vitendo hivyo wakati wa uchaguzi, Takukuru ambayo ina watumishi wasiozidi 4,000 nchi nzima, imejipanga kuvikomesha katika uchaguzi ujao kwa kutumia wadau wakiwemo viongozi wa dini.

“Pia, uelewa mdogo wa wananchi kuhusu umuhimu wa kupigakura na athari za rushwa ni mdogo. Utakuta wananchi wanapewa chumvi, kanga bila kuelewa madhara yatakayompata katika kipindi cha miaka mitano baada ya kupokea rushwa hizo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, James Ruge amesema rushwa siyo tu ni kosa la kisheria, pia ni kosa la kiimani na kimaadili katika jamii huku akiwaomba viongozi wa dini mkoani humo kusaidia jitihada za kuzuia vitendo hivyo katika jamii kwa njia ya elimu.

“Viongozi wa dini ni muhimu kwa sababu wanamchango kwenye mapambano dhidi ya rushwa katika nyumba za ibada. Mkoa wa Mwanza una watu wengi takribani milioni 3.6, kwa hiyo tunaamini mafunzo haya kwa viongozi wa dini tutakuwa na matokeo ya uchaguzi yasiyochangiwa na rushwa,” amesema Ruge.

Amesema rushwa ikiendekezwa katika uchaguzi itashamiri na kuchangia jamii kupata viongozi wasiyofaa na wasiyoweza kusimamia rasilimali za nchi na kuwaletea wananchi maendeleo huku akiwataka wananchi kutokubaliana na vitendo hivyo badala yake wawafichue wagombea watakaobainika kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amesema jitihada za kutokomeza rushwa kwenye uchaguzi zitafanikiwa kwani tayari vita hiyo imekabidhiwa kwa viongozi wa dini kwa kile alichodai mahubiri yatakayofanyika katika makanisa na misikiti mkoani humo yatatawaliwa na elimu ya rushwa.

Pia, amesema watatumia mafunzo hayo kuhamasisha waumini kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kuanzia kujiandikisha, kuchukua fomu, kupiga kura na kuimarisha amani wakati wote wa uchaguzi huo.

“Hii vita ni ya kwetu, tutumieni na sisi tutahakikisha kuanzia sasa kwenye mahubiri yetu rushwa itakuwa kipaumbele kwa sababu hata vitabu vya dini vinakataza rushwa. Nikitolea mfano kwenye Q’uran rushwa ni miongoni mwa makosa yenye adhabu kubwa kuliko kawaida,” alisema Kabeke ambaye ni Sheikh wa Mkoa wa Mwanza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekelwa ameitahadharisha jamii kuwa wagombea wenye nia ya kutoa rushwa huwa na tabia ya kujisogeza kwa wapiga kura uchaguzi unapokaribia lakini wakishachaguliwa hutokomea.

Askofu Sekelwa ameitaka jamii kuwa makini na wagombea wa aina hiyo kwa kuripoti Takukuru wanapobaini dalili za kutokea vitendo vya rushwa.

Kupitia mafunzo hayo, viongozi wa dini mkoani Mwanza wameafikiana kutumia majukwaa ya ya kidini kutoa elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa, viongozi wa dini kuhamasisha waumini kuwakataa wagombea wanaotoa rushwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Related Posts