VIDEO: Mtoto anayelea wadogo zake watano akabidhiwa mjengo wa kisasa

Rombo. Siku chache baada ya Mwananchi kuripoti habari ya mwanafunzi wa darasa la sita, James Efram (14) anayelea wadogo zake watano kutokana ugumu wa maisha baada ya baba yao kufariki dunia mwaka 2011, jana Agosti 30, 2024 amekabidhiwa nyumba ya kisasa na  shirika linalosaidia wanaoishi katika mazingira magumu.

James ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Mamonjo, iliyopo wilaya ya Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro yeye na wadogo zake watano pamoja na mama yao mzazi,  walikuwa wakilala chini kutokana na kukosa vitanda na magodoro huku wakiishi kwenye nyumba mbovu ya dongo isiyo na paa.

Kutokana na ugumu huo wa maisha kulimfanya mwanafunzi huyo kubeba jukumu la kuwalea wadogo zake hao pamoja na mama yake mzazi,  ambaye ana changamoto ya afya ya akili hali ambayo ilimfanya wakati mwingine kukosa masomo darasani ili kwenda kutafuta chochote kitu mtaani.

Hata hivyo,  pamoja na changamoto hiyo aliyokuwa akiipitia James hakuwahi kufeli darasani na amekuwa akishika nafasi ya kwanza hadi ya tatu darasani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa nyumba hiyo, Mbunge wa Rombo ambaye ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amelishukuru shirika la Glads welfare Organization pamoja na walimu wa shule anayosoma kwa kumuibua mwanafunzi huyo.

“Nimpongeze mwalimu aliyemuibua mwanafunzi huyu, hasa pale walipombaini James hayupo shuleni wakamfuatilia nyumbani kwake kujua changamoto ni nini na baadaye   wakagundua kwamba anahitaji msaada, walichofanya cha kwanza walichanga Sh5, 000 kupitia mishahara yao kuhakikisha wanamsaidia,” amesema Profesa Mkenda.


Mtoto anayelea wadogo zake watano akabidhiwa mjengo wa kisasa

Amesema walichokifanya walimu hao kumsaidia mwanafunzi huyo ni jambo kubwa la kuigwa na watu wengine na kwamba tatizo hilo lipo maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Hili sio jambo la kawaida hata kidogo, hili walilolifanya walimu ni zaidi ya majukumu yao, kuingia mfukoni na kutoa fedha zao hili ni jambo kubwa sana , nawashukuruni sana walimu wangu na naomba tumpongeze kwa kumtafuta huyu Glady Welfare organization na kuweza  kumsaidia James na familia yake,” amesema Profesa Mkenda

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya nyumba hiyo, Mkurugenzi wa Glady welfare Organization, Glady Lyamuya amesema baada ya kupigiwa simu na walimu wa shule anayesoma mwanafunzi huyo, alifika nyumbani hapo kuona mazingira ya familia hiyo hali ambayo ilimfanya abaki kwenye familia hiyo kuwasaidia kutokana na mazingira waliyokuwa wakilala na kwamba ni kama walikuwa wakiishi nje.

“Ndugu zangu nilipopigiwa simu na kupewa taarifa ya James na familia yake mimi kama mzazi baada ya kufika hapa nilishindwa kuondoka na nipo na hii familia tangu nimekuja kuwaona siku ya kwanza nikisimamia ujenzi na kuhakikisha mahitaji mengine yote yanapatikana hapa. Hii  familia imepitia maisha magumu sana lakini  Mwenyezi Mungu amewasaidia na wataingia katika nyumba hii mpya,” amesema Lyamuya

Muonekano wa nyumba ya udongo aliyokuwa akilala awali James Efram (14) na wadogo zake pamoja na mama yake mzazi.

Amesema tangu waanzishe taasisi hiyo wamejenga nyumba tisa  zikiwemo nyumba tatu Mkoa wa Kilimanjaro ambazo  zinasaidia familia ambazo hazina uwezo.

Akitoa mahubiri wakati akibariki nyumba hiyo mpya, Paroko wa Parokia ya Usseri, Padre Amedeus Mtui, ameitaka jamii kuendelea kuwa na upendo na mshikamano na kuhakikisha wanashirikiana kwa kila jambo pale ambapo mwanajamii anapopatwa na changamoto za kidunia.

Related Posts