Waajiri watakiwa kutoa taarifa za wanaoumia kazini

Arusha. Serikali imewaagiza waajiri kote nchini kutoa taarifa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), zinazohusu wafanyakazi wao wanaopata ajali, ugonjwa au kifo katika maeneo yao ya kazi, ili waweze kupatiwa stahiki zao kwa wakati kwa mujibu wa sheria.

Hayo yamebainishwa Agosti 30, 2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, akizungumza katika kikao kazi kati ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na maofisa kazi kote nchini.

Amesema ni muhimu waajiri kusimamia maslahi ya wafanyakazi wao sehemu za kazi, ili kuondoa malalamiko ikiwemo wanaopata majanga wakiwa kazini.

“Ninatumia fursa hii kutoa rai kwa waajiri kote nchini kutoa taarifa katika ofisi za WCF za matukio ya ajali, ugonjwa au kifo kinachotokana na kazi na kujisajili na kuwasilisha michango kwa wakati,” amesema.

Waziri huyo amesema ni jukumu la watendaji hao kusimamia sheria ya Taasisi za Kazi sura ya 300 na Sheria ya fidia kwa wafanyakazi sura ya 263 kwa kuhakikisha waajiri wanatekeleza.

Amesema baadhi ya maofisa kazi wa mikoa wamekuwa wakilalamikiwa kutotatua migogoro na malalamiko ya wafanyakazi, jambo ambalo limekuwa likitoa taswira mbaya kwa Serikali.

Ridhiwani amesema amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi kutotendewa haki katika maeneo yao ya kazi.

“Naomba niwakumbushe hamkupewa ofisi kuwa vitanda na nyumba zenu za kuishi. Nataka nisikie mnatatuaje malalamiko ya wafanyakazi na siyo kuwapa majibu ya kashfa kama baadhi yenu ambavyo mmekuwa mkiwajibu wafanyakazi,” ameongeza.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa mfuko huo, Dk John Mduma amesema wamefanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa kiutendaji na kwa sasa huduma za mfuko huo zinatolewa kwa njia ya mtandao kwa zaidi ya asilimia 90.

Kamishna wa Kazi nchini, Suzan Mkangwa amesema ofisi hiyo imekuwa ikishirikiana na mfuko wa WCF katika kuhakikisha malalamiko ya wafanyakazi yanatolewa kwa wakati.

Related Posts