Bukoba. Baadhi ya wavuvi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera walioshiriki kuokoa majeruhi 24 kwenye ajali ya ndege ya Pricision Air, wameelezea wasiwasi wao juu ya matumizi ya fedha walizopewa kama shukrani kwa kuhoji matumizi ya Sh30 milioni walizopewa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Ajali hiyo ilitokea Novemba 6, 2022 na kusababisha vifo vya watu 19, majeruhi 24.
Wasiwasi wa matumizi ya pesa zilizotolewa wakati huo umeibuka katika mkutano wao ambapo viongozi walisoma taarifa ya mapato na matumizi ya fedha hizo, huku wavuvi waliohudhuria kikao hicho wakibaini kuwa kiwango walichosomewa kimezidi fedha waliyopewa yaani Sh30 milioni.
Katika kikao hicho, mvuvi Elizeus Kamugisha amesema hesabu za matumizi ya fedha hizo haijawekwa sawa wanahitaji kujua viongozi walifanya nini kwani malengo yao walipanga kuanzisha miradi miwili mikubwa ya ununuzi wa boti na fedha nyingine wafanyie ununuzi wa vifaa vingine vya uvuvi.
Ameongeza kuwa hawezi kuwaamini tena viongozi wa kikundi hicho kwa sababu katika taarifa waliyosomewa na katibu siyo sahihi ukilinganisha na matumizi ya fedha yote.
“Dukuduku langu linakuja pale ninaposikia kuwa milioni 30 zimetumika katika ununuzi wa boti mbili halafu kuwa kuna na matumizi mengine, Serikali tunaomba itusaidie kwa hili,” amesema.
Katibu wa kikundi cha wavuvi mwalo wa nyamkazi, Antidius Doroteca akisoma taarifa ya mapato na matumizi ya fedha hizo, amesema zilitumika katika ununuzi wa boti mbili.
Doroteca, amesema mradi wa kwanza wa ununuzi wa boti moja ya Mv Dk Samia Suluhu Hassan uligharimu kiasi cha Sh15.8 milioni na mradi wa pili ni ununuzi wa boti ya Mv Miembeni uliogharimu kiasi cha fedha Sh11.7 milioni.
“Boti hizo kama mlivyosikia katika ununuzi zinafanya kazi ya kuingiza kipato cha kikundi katika mwalo wa Nyamkazi ziwa Victoria na hayo ndiyo matumizi ya fedha zetu na kuna fedha nyingine zilifanya kazi nyingine ni zaidi ya Sh30 milioni,” amesema.
Ofisa uvuvi Mkoa wa Kagera, Efraz Mkama katika kikao hicho amewahakikishia wavuvi hao kuwa hoja na changamoto zote walizoziwasilisha, atahakikisha zinawafikia viongozi wa juu na kutafutiwa ufumbuzi.
“Viongozi wenu wametoa taarifa na kwa upande wenu mmetoa mapendekezo sisi kama Serikali tumeyachukua tutahakikisha tunayafanyia kazi,” amesema.