Wanafunzi watatu, dereva wafa ajalini, Manyara

Babati. Wanafunzi watatu na dereva wamefariki dunia kwa ajali ya gari wilayani Babati mkoani Manyara, baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani ajali hiyo imehusisha gari la mizigo aina ya scania kugongana na basi dogo aina ya coaster.

Kamanda Makarani amesema ajali hiyo imetokea alfajiri ya leo Agosti 31 mwaka 2024 eneo la Gajal wilayani Babati.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni gari hiyo aina ya scania kuligonga basi hilo dogo lililokuwa likitokea wilayani Hanang’ likielekea jijini Arusha likiwa na wanafunzi 33.

“Dereva wa lori alikuwa mzembe kwani alishindwa kuwa makini barabarani na kuligonga basi hilo dogo na kusababisha vifo hivyo,” amesema kamanda Makarani.

Amesema wanafunzi watatu waliokuwa kwenye basi hilo dogo walifariki dunia pamoja na dereva aliyekuwa akiwaendesha watoto hao.

“Wanafunzi hao waliokuwa kwenye hilo basi dogo walikuwa wanatoka shule ya sekondari Endasak wanaelekea jijini Arusha baada ya shule  kufungwa hivi karibuni.

Baadhi ya wakazi wa eneo la Gajal wilaya ya Babati mkoani Manyara wakiwa eneo la ajali iliyosababisha vifo vya wanafunzi watatu na dereva wa basi dogo aina ya Coaster. Picha na Joseph Lyimo

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga ametoa pole kwa wanafunzi, walimu, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kutokana na ajali hiyo.

“Tunamuomba Mwenyezi Mungu, awape nafuu na uponyaji wa haraka majeruhi wote wa ajali hiyo ambayo imesababisha vifo vya watu wanne,” amesema Sendiga.

Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk Andrew Method amethibitisha kutokea vifo hivyo vinne.

Dk Method amesema majeruhi 30 wa ajali hiyo wamepokelewa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa huo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwemo Athuman Rizi, wamemlaumu dereva wa lori hilo kwa kusababisha vifo hivyo vya wanafunzi hao na dereva wao.

“Wazazi wanawasubiria watoto wao wafike nyumbani ila wanakatishwa maisha yao kwa uzembe wa mtu mmoja ambaye hakuwa makini kwenye uendeshaji wake,” amesema Rizi.

Related Posts