Wanne wafariki ajalini wakitoka harusini

Dodoma. Watu wanne wamefariki dunia baada ya lori aina ya Scania lilobeba mafuta ya petroli kugongana uso kwa uso na basi aina ya Coaster iliyobeba ndugu waliokuwa wakitoka katika sherehe ya harusi Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishana Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi, George Katabazi amesema ajali hiyo ilitokea leo Agosti 31, 2024, saa 12.00 asubuhi katika eneo la Manchali Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Amesema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya coaster lililokuwa likitokea Dodoma kuelekea Morogoro na lori aina ya Scania lililokuwa limebeba mafuta ya petroli, likitokea Morogoro kuelekea Dodoma.

Amesema chanzo cha ajali ni dereva wa gari la abiria kutochukua tahadhari wakati akijaribu kulipisha basi lililokuwa mbele yake na hivyo kusababisha kugongana uso kwa uso na lori.

Amesema watu watatu akiwemo dereva wa coaster na abiria wawili waliokuwa katika gari hilo walifariki dunia katika eneo la ajali,  wakati  mwingine alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

Amesema ajali hiyo imesababisha majeruhi 16 ambao wamelazwa hospitali wakiendelea na matibabu.

“Nipende kutoa rai kwa watumiaji barabara kuchukua tahadhari ya hali ya juu kwa sababu ajali hii imetokana na makosa ya kibinadamu ama uzembe. Barabara imenyooka haina kona na inaonekana kwa uwazi ina maana dereva wa coaster angechukua tahadhari wakati wa kulipita gari jingine asingeweza kupata ajali ya namna hiyo,” amesema.

Amesema watumiaji wa barabara wasipozingatia kuchukua tahadhari wakati wa kuyapita magari mengine, watasababisha ajali.

Amesema Jeshi la Polisi litakuwa kali kwa kuimarisha doria katika barabara kuu kwa kutumia magari na askari kwenye barabara hizo kuhakikisha ajali za namna hiyo hazitokei.

Naye Daktari katika kitengo cha magonjwa ya dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Florence Ramson amesema kuanzia saa 2.00 asubuhi walianza kupokea majeruhi na kuwa hadi jana mchana walikuwa wakiendelea kuwapokea.

Amesema walipokea jumla ya majeruhi 13 na kuwa kati ya hao saba ni wanawake na sita ni wanaume.

“Watoto wako watatu, kuna mtoto wa miaka 10, mitano na mtoto mdogo wa miezi mitano. Wagonjwa  wengi wanaendelea vizuri lakini watatu walienda moja kwa moja chumba cha operesheni lakini wawili pamoja na mtoto mmoja wako katika chumba cha uangalizi maalumu,” amesema.

Amesema katika kitengo cha magonjwa ya dharura wamebakiza wagonjwa watatu ambao wamepata majeraha mdogo madogo na kuwa baadaye watawapeleka wodini kwa ajili ya uangalizi zaidi.

Walikuwa wakitoka katika harusi

Mmoja wa majeruhi aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Abdallah Salehe Wangaza alisema gari hilo lilibeba wanafamilia waliotokea Isaka, Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga wakielekea jijini Dar es Salaam.

“Tulikuwa kama familia tulikuwa tunatoka Kahama kwa ajili ya sherehe ya harusi ya ndugu yetu na huyu anayeoa ni ndugu yetu,” amesema.

Amesema walianza safari saa 2.30 usiku na ilipofikia saa 12 asubuhi walipata ajali baada ya dereva wa lori kuhama njia na kuligonga gari walilokuwa wamepanda.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aliyetembelea majeruhi katika Hospitali ya Uhuru iliyopo Wilayani Chamwino, ametoa rai kwa madereva kuzingatia taratibu za uendeshaji vyombo vya moto ili kuepusha ajali zinazopoteza maisha ya watu.

“Tumetoka kumaliza maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama ambayo ilikuwa na kauli mbiu endesha salama ufike salama, hivyo niwasihi madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani. Mfano ajali hii ni uzembe katika kulipita gari,” amesema.

Related Posts