DEREVA Yassin Yasser amesema yuko kamili kwa ajili ya kutetea ubingwa wake wa mbio za magari ya Iringa baada ya gari yake Ford Fiesta R5 kusukwa upya kufuatia ajali mbaya wakati wa mashindano mbio za magari ya kimataifa nchini Kenya.
Nasser na msoma ramani wake Ali Katumba ndiyo mabingwa wa taifa wa mbio za magari kwa msimu wa mwaka 2023 na miongoni mwa washiriki 24 waliokwisha thibitisha ushiriki wao kabla ya mashindano kuanza kutimua vumbi Septemba 14 na 15 katika barabara za Iringa vijijini, kwa mujibu wa katibu wa chama cha mbio za magari Iringa(IMSC), Maneno Robert.
“Kila kitu kipo tayari na hadi mwishoni mwa juma hili madereva 12 na wasoma ramani 12 wamekwisha thibitisha kuja Iringa wakati tukitegemea wengine zaidi kuendelea kuthitibisha,” alisema katibu huyo wa IMSC.
Iringa inaandaa raundi ya pili ya ubingwa wa mbio za magari wa taifa(NRC) mwaka huu baada ya mkoa wa Tanga kufungua msimu kwa mbio za kilomita 155 mwezi Julai mwaka huu.
Kuwepo kwa Nasser na Ford Fiesta R5 kunafanya mashindano ya Iringa kuwa ni vita ya Ford Fiesta dhidi ya vinara wa raundi ya kwanza, Mitsubishi Evos.
Nasser alipata ajali kubwa wakati wa mbio za magari ya kimataifa ya Kenya iliyopelekea gari yake kuharibika vibaya. Lakini baada ya marekebisho ya kina, gari yake iko tayari kwa mbio za magari ya Iringa, kwa mujibu wa katibu Robert.
Hata hivyo Nasser atakuwa na kibarua kizito mbele ya mwenyeji Ahmed Huwel ambaye pia ataingia mashindanoni na Ford Fiesta Proto.
Ushiriki wa madereva hawa kunaoneka kuleta upinzani kwa timu ya madereva wa Mitsusbishi ambayo ilitawala katika raundi ya ufunguzi kupitia mshindi wake Randeep Birdi wa Dar es Salaam na mshindi wa pili, Gurpal Sandhu wa Arusha.
Kwa mujibu wa afisa wa IMSC, mbio za magari za Iringa zitaanzia katika uwanja wa Samora katikati ya mji wa Iringa ambako kutafanyika mbio fupi za Super Special Stage ili kuamua ni dereva yupi aondoke wa kwanza siku ya Jumapili, tarehe 15 Septemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa Robert, Shamba la Mzee Huwel lililopo eneo la Kikongoma, kiasi cha kilomita 35 magharibi ya mji wa Iringa, ndiyo eneo kuu la mashindano ambayo njia zake zitapitia pia maeneo mengi ya kiutalii na kihistoria ya mkoa wa Iringa.