Dar es Salaam. Kamati Kuu Maalumu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imewateua makada wake 10 kugombea ubunge wa Afrika Mashariki (EALA), kurithi nafasi iliyoachwa wazi na Dk Shongo Sedoyeka aliyefariki dunia Juni 13, 2024.
Hata hivyo, uamuzi huo wa kamati kuu umewakata makada wengine 37 waliotia nia kuomba ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kugombea ubunge wa EALA.
Taarifa ya uteuzi wa wagombea hao, imetolewa leo Jumapili, Septemba 1, 2024 na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla baada ya kikao cha sekretarieti ya chama hicho na kamati kuu maalumu iliyoketi leo.
Amewataja walioteuliwa ni Gladness Salema, Maria Sebastian, Queenelizabeth Makune, Ester Chaula, Profesa Neema Kumburu, Lucia Pande, Fatuma Kange, Hawa Mkwela, Fatma Msofe na Theresia Dominic.
Hatua ya kupigiwa kura kwa wagombea hao, Makalla amesema itafanyika kesho Jumatatu Septemba 2, 2024 na kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM, saa 8 mchana, jijini Dodoma.
Hilo litafuatiwa na uchaguzi wa mbunge huyo utakaofanyika Septemba 5, 2024, utakaohusisha wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.