Jana Jumamosi, Aishi Salum Manula alirejea kwenye milingoti mitatu ya Simba tangu mara ya mwisho aonekane katika majukumu yake Machi 6 mwaka huu.
Manula ambaye amekuwa nje ya kikosi cha Simba kwa takribani miezi mitano, alikuwa akiuguza majeraha ya nyonga, lakini baada ya kupona alichelewa kujiunga na wenzake baada ya kuwepo sintofahamu kutokana na nafasi yake kikosini hapo.
Iliripotiwa kwamba, kipa huyo ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu anahitajika na Azam, lakini hadi usajili unafungwa dili hilo halikufanyika.
Kabla ya juzi hajakaa katika milingoti mitatu ya Simba katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Al Hilal, kipa huyo hakudaka mechi yoyote ile kikosini hapo iwe ya kirafiki au kimashindano.
Kipa huyo mchezo wa mwisho kucheza ndani ya Simba ulikuwa wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons uliofanyika Machi 6 kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ambapo aliruhusu mabao mawili Simba ikifungwa 2-1.
Baada ya hapo, amekosa jumla ya mechi 27 zikiwamo 23 za kimashindano na nne za kirafiki.
Juzi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Al Hilal ya Sudan uliochezwa Uwanja wa KMC uliopo Mwenge Dar es Salaam, alianza kikosi cha kwanza na kufanikiwa kucheza kwa dakika 45.
Ndani ya dakika hizo 45 ikiwa ni mara ya kwanza anaonekana katika milingoti mitatu ya Simba akicheza mechi, alionesha kiwango kilichowaridhisha Wanasimba.
Licha ya kwamba hakupata mashambulizi mengi langoni mwake kutokana na kulindwa vizuri na mabeki wake hasa wale wa kati, Chamou Karaboue na Che Malone Fondoh, lakini alifanya sevu tatu matata sana.
Sevu ya kwanza ilikuwa dakika ya 12 ambapo alifanikiwa kumzuia nyota wa Al Hilal, Aime Tendeng akiwa anatazamana naye kisha zingine mbili zilitokea mfululizo dakika ya 32 akianza kuokoa ya Adama Coulibaly kisha ile ya Pape Abdou Ndiaye ambapo mashabiki walionekana kuridhishwa na kiwango hicho.
Katika dakika hizo 45 kabla ya kipindi cha pili hajampisha Hussein Abel, Manula aliondoka na clean sheet, huku akipiga pasi 23. Kati ya hizo alipoteza tatu ambazo zote ni zile pasi ndefu, ikionekana ana tatizo la kupiga pasi ndefu zinazoweza kuwafikia walengwa.
Manula aliumia Machi 22 akiwa anaitumikia timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika michuano maalumu ya Fifa Series iliyofanyika Baku, Azerbaijan.
Katika mchezo dhidi ya Bulgaria uliochezwa Dalga Arena ambapo Taifa Stars ilipoteza kwa bao 1-0, Manula alitoka uwanjani dakika ya 31 nafasi yake ikachukuliwa na Kwesi Kawawa.
Baada ya kuumia, Manula amezikosa mechi 16 za ligi kuu zikiwamo 14 za msimu uliopita na mbili msimu huu. Mechi hizo ni Coastal Union, Singida Fountain Gate, Mashujaa,
Ihefu, Yanga, Namungo, Mtibwa Sugar, Tabora United, Azam, Kagera Sugar, Dodoma Jiji, Geita Gold, KMC na JKT Tanzania, hizi za msimu uliopita wakati msimu hii ni Tabora United na Fountain Gate.
Pia mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya Al Ahly. Moja ya Kombe la FA dhidi ya Mashujaa na mbili za Kombe la Muungano dhidi ya KVZ na Azam.
Ulivyomalizika msimu wa 2023/24, Manula akakosekana katika pre-season iliyofanyika Misri ambapo Simba ilicheza mechi tatu dhidi ya El-Qanah Egypt, Telecom Egypt na Al-Adalah FC. Katika Tamasha la Simba Day hakuwepo wakati Simba ilipocheza dhidi ya APR. Akakosekana pia mechi mbili za Ngao ya Jamii msimu huu dhidi ya Yanga na Coastal Union.
Kabla ya juzi kucheza mechi dhidi ya Al Hilal, Agosti 16 mwaka huu Manula kwa mara ya kwanza alionekana mazoezini akijumuika na wenzake katika mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa KMC wakijiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United ingawa siku ya mechi hakuwepo hata benchi.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema: “Aishi bado ni mchezaji wa Simba na ataendelea kuwa mchezaji wa Simba akiutumikia mkataba wake wa mwaka mmoja. Kwa sasa amepona na amerejea kwenye timu.”