Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Longido (DC), Marco Ng’umbi baada ya kuhudumu kwa mwaka mmoja na miezi minane katika wilaya hiyo.
Ingawa taarifa ya Ikulu iliyotolewa jioni ya leo Jumapili, Septemba mosi, 2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga, haikuweka wazi sababu za kutenguliwa kwake, uamuzi huo umekuja muda mfupi baada ya kusambaa kipande cha video inayomwonyesha akizungumza mambo kadhaa kuhusu uchaguzi wa mwaka 2020.
Katika picha hiyo jongefu ya dakika 1.32, Ng’umbi anasikika akiwaeleza watu aliowataja mara kadhaa kuwa ni madiwani kwamba ushindi wao katika uchaguzi huo si ujanja wao, bali ni nguvu ya Serikali.
Alikwenda mbali zaidi na kueleza hata waliopita bila kupingwa ni kazi iliyofanywa na Serikali na sio ubora wa wagombea husika.
“Kama kuna mtu ambaye si mwoga ni mimi, wote hapa madiwani mwaka 2020 hayupo diwani aliyepiga kampeni hapa. Sasa yale mazingira ya mwaka 2020 si kwamba yalikuja yenyewe moja kwa moja kwa sababu ninyi mlikuwa wagombea bora sana.
“Ni mazingira ambayo yalikuwa yametengenezwa na Serikali na Serikali ndiyo iliyoifanya kazi ile ya wewe kupita bila kupingwa. Kuna watu unafahamu kilichotokea huko kwenye pori anasema mimi sijui na mimi nilihusika kwenye majimbo fulani fulani,” alisikika katika kipande hicho cha video.
Wakati Ng’umbi akikumbwa na utenguzi huo, Kamati Kuu ya CCM nayo imewavua uongozi viongozi wake wawili, akiwemo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT) Mkoa wa Lindi, Palina Ninje.
Pamoja na Palina, mwingine aliyevuliwa uongozi ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo, Abdul Zahoro.
Hatua ya kuvuliwa kwa viongozi hao wa CCM, imetangazwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alipotoa taarifa ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika leo.
Katika taarifa yake hiyo, Makalla amesema uamuzi huo wa kamati kuu, umetokana na viongozi hao kukiuka maadili ya uongozi ya chama hicho.
Wakati huohuo, kamati kuu hiyo maalumu imewateua wanachama 10 kuwania nafasi ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kati ya 47 waliojitokeza kuwania kuteuliwa.
Walioteuliwa kesho Jumatatu, watapigiwa kura na kikao cha kamati ya wabunge wa CCM jijini Dodoma na Septemba 5, 2024 kutakuwa na uchaguzi wa kumpata mbunge mmoja kwa kuchaguliwa na Bunge la Tanzania.
Walioteuliwa ni Gladness Salema, Maria Sebastian, Queenelizabeth Makune, Ester Chaula, Neema Kumburu, Luda Pande, Fatuma Kangwe, Hawa Mkwela, Fatma Msofe na Theresia Dominic.
Kwa pamoja wanawania nafasi iliyoachwa na Dk Shongo Sedoyeka aliyefariki dunia Juni 13, 2024.