BAADA ya kusepa Simba, mshambuliaji Freddy Kouablan amerejea nchini kimya kimya, lakini akashtua kujifua na mastaa wa Yanga.
Freddy ambaye alitua Simba dirisha dogo msimu uliopita akitokea Green Eagles ya Zambia akiwa amefunga mabao 11 yaliyomfanya awe Mfungaji Bora mwishoni mwa msimu wakati akiwa Msimbazi, aliondoka Simba hivi karibuni kumpisha Leonel Ateba kutoka USM Alger ya Algeria.
Muivory Coast huyo msimu uliopita Simba alimaliza kwa kufunga mabao sita katika ligi na mengine mawili ya Kombe la Shirikisho na jingine moja la Kombe la Muungano, lakini juzi aliibukia ufukweni akiwa sambamba na mastaa wa Yanga.
Mshambuliaji huyo alionekana akijifua fukwe za Kawe na mastaa watatu wa Yanga akiwemo kipa Djigui Diara, kiungo Pacome Zouzoua na beki Yao Kouassi ambao wawili hao ni raia wenzake wa Ivory Coast.
Kufuatia picha hiyo Mwanaspoti lilimtafuta ambapo amejibu kifupi kuwa yupo nchini kwa ratiba zake binafsi.
Freddy alipoulizwa na Mwanaspoti, alifunguka ametua nchini akitokea Algeria alikokwenda kumalizana na moja ya klabu za huko kisha kurejea kujifua ili kujiweka fiti.
“Nipo hapa nina siku chache, nimekuja kwa mambo yangu binafsi,(Pacome, Yao na Diarra) ni rafiki zangu waliokuwa wanakwenda mazoezini nikaona niende nao,” amesema Freddy na kuongeza;
“Wakati wa mapumziko kama hivi huwa tunakuwa wote, hata wakati nikiwa Simba, unajua Kuna maisha baada ya timu tulizokuwa tunazitumikia.”
Aidha alipoulizwa kama ataweza kujiunga na Yanga, Freddy akaishia kucheka kisha akasema Yanga ni timu kubwa lakini kwas asa siwezi kusema lolote.