Gamondi, Mzize wana siri nne

WAKATI mashabiki wa Wydad Casdablanca ya Morocco wakivamia ukurasa wa straika chipukizi wa Yanga, Clement Mzize anayehusishwa na timu hiyo sambamba na ile ya Kazier Chiefs ya Afrika Kusini, kocha mkuu wa klabu hiyo, Miguel Gamondi amebainisha mambo manne aliyonayo kwa mchezaji huyo.

Mashabiki wa Wydad walivamia ukurasa wa Instagram wa Mzize wakimkaribisha katika timu hiyo baada ya kuposti ujumbe wake akiandika ‘Kesho ni fumbo usimdharau mtu kwa uwezo au udhaifu alionao’, na mashabiki kuchangia ujumbe chini ya chapisho hilo wakimkaribisha kuichezea klabu hiyo inayodaiwa kumnyemelea.

Lakini hayo yakiendelea ikiwa ni siku chache tangu Mzize afunge bao la pili wakati Yanga ikiizamisha Kagera Sugar  mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara, Gamondi ameanika mambo manne.

Katika mambo hayo kocha huyo amesema yanatosha kumfanya Mzize kuchukua uamuzi sahihi kwa ajili ya mustakabali wa ukuaji wake kisoka.

Ipo hivi. Mzize kwa siku za hivi karibuni amekuwa akihitajika na Wydad AC na Kaizer Chiefs ambazo zimeweka mzigo wa kutosha mezani ili kumng’oa kinda huyo.

Inaelezwa Kaizer iliweka Dola 200,000 ambazo ni sawa na Sh542.3 milioni, ofa ambayo Yanga imeitupilia mbali  kutoka klabu anayoinoa kocha wa zamani wa Jangwani, Nasreddine Nabi aliyempandisha Mzize kikosi cha wakubwa, huku Wydad inayofundishwa na Rhulani Mokwena ikiweka Dola 100,000 (takriban Sh271.1 milioni).

Hata hivyo, inaelezwa kuwa mabosi wa Yanga wameweka dau kubwa kwa klabu inayomtaka Mzize kwa sasa ambapo italazimika kwenda mezani ikiwa na Dola 1 milioni (zaidi ya Sh2 bilioni), huku ikidaiwa ameshasainishwa mkataba mpya wa miaka miwili unaomuweka klabuni hapo hadi 2027.

Gamondi aliye na Mzize kwa msimu wa pili, anaamini bado nyota huyo anahitaji kuwepo katika timu hiyo ili kuendelea kukua kisoka na siyo kuondoka wakati huu.

Kocha huyo Muargentina amebainisha kuwa amekuwa akikaa na kuzungumza na mchezaji huyo ili kumshauri masuala mbalimbali ya kisoka ambapo ameyataja mambo manne baada ya uwepo wa ofa hizo.

Mambo hayo aliyoyabainisha Gamondi amegusia utamaduni, lugha, utayari wa mchezaji kuondoka na hatima yake kisoka.

“Clement ni kama mwanangu. Nilikuwa mtu wa kwanza kumtetea na kumlinda. Kwa sasa anajisikia vizuri kuwa Yanga. Watu wanampenda ndani ya klabu, pia kama kocha namuelewa vizuri, nafikiri naweza kumsaidia sana kukua,” alisema Gamondi.

“Yeye mwenyewe alisema hata msimu uliopita bado hajajiandaa kuondoka. Najua vizuri jinsi inavyokuwa ngumu unapokuwa mgeni sehemu fulani. Hujui lugha wala utamaduni wao, inakuwa ngumu kwako. Kwangu ilikuwa uamuzi wa busara kwake kuongeza mkataba na Yanga kwa sababu kama nilivyomwambia yeye ni mchezaji mzuri sana. Hata kwetu itakuwa vizuri kumuuza kwa pesa nyingi na kwenda klabu kubwa. Sitaki kumuweka Clement abaki hapa kama hana furaha, lakini sasa anafurahi.”

Kaizer inanolewa na Nabi ambaye alikuwa kocha wa kwanza kumpandisha Mzize kucheza timu ya wakubwa ya Yanga akitokea kikosi cha vijana.

Katika msimu wa 2022/23, Mzize alicheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu Bara chini ya Kocha Nabi akifunga mabao matano huku akifunga sita katika Kombe la FA na kushika nafasi ya pili kwa waliofunga mabao mengi nyuma ya kinara Andrew Simchimba aliyemaliza na saba.

Msimu uliopita wa 2023/24, Mzize aliibuka mfungaji bora wa Kombe la FA akifunga mabao matano, huku katika Ligi Kuu alitupia sita na kuasisti matano.

Nabi ambaye alikiona kipaji cha mshambuliaji huyo tangu akiwa timu ya vijana ya Yanga, anamchukulia Mzize atakuja kuwa msaada mkubwa ndani ya timu yake.

Mzize mwenye umri wa miaka 20, bado yupo katika ukuaji kisoka hivyo kwa namna ya upambanaji wake ndani ya uwanja na uwezo wa kuwasumbua mabeki wa timu pinzani, ndiyo silaha yake kubwa inayombeba.

Kwa upande wa Mokwena, alianza kuvutiwa na Mzize tangu akiwa anaionoa Mamelodi Sundowns ambayo msimu uliopita ilicheza dhidi ya Yanga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mechi zote mbili dhidi ya Mamelodi, Mzize alicheza kwa dakika 110.

Aina ya uchezaji wa Mzize akitokea pembeni na wakati mwingine akicheza eneo la kati katika ushambuliaji, umeonekana kuwavutia makocha wengi kwani mshambuliaji huyo amekuwa msaada mkubwa katika upatikanaji mabao.

Mbali na hilo, Mzize ana uwezo mkubwa wa kutumia vizuri miguu yake miwili kitu ambacho washambuliaji wengi hawana.

Related Posts